Lumbanga atinga kesi ya Mahalu
February 28, 2008
KESI ya kuhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Costa Ricky Mahalu na mwenzake, imeanza kusikilizwa jana kwa upande wa mashitaka kumwita aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Martens Lumbanga. Akitoa ushahidi wake jana, Lumbanga, ambaye kwa sasa ni Balozi wa kudumu katika Umoja wa Mataifa, Geneva, Uswisi, aliieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwa Balozi Mahalu alikwenda ofisini kwake kumuomba msaada kwa ajili ya ununuzi wa jengo la ubalozi nchini Italia.
Akitoa ushahidi huo mbele ya Hakimu Mkuu wa makahama hiyo, Sevangilwa Mwangesi, shahidi huyo alidai Mahalu alimweleza kuwa kiasi kilichotengwa cha sh bilioni moja hazitoshi kununua jengo hilo, hivyo awasiliane na mmiliki wa jengo ili wasilipe kodi.
“Kwa kutumia nafasi yangu nilimshauri Mahalu kuwa jukumu hilo si la Serikali ya Tanzania, bali awasiliane na mmiliki wa jengo hilo na serikali ya nchi hiyo iwapo kuna uwezekano wa kufanya hivyo - kutolipa kodi hiyo,” alieleza.
Hata hivyo, alieleza kuwa hafahamu kuwapo kwa mikataba miwili ya ununuzi wa jengo hilo, kwani taarifa hizo amezisoma kwenye vyombo vya habari.
Akihojiwa na wakili wa utetezi, Alex Mgongolwa, kuhusu barua aliyoandika Balozi Mahalu kuhusu mikataba hiyo, shahidi huyo alieleza kuwa anaufahamu mkataba mmoja ambao ni wa sh bilioni moja.
Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya wakili Mgongolwa na shahidi huyo.
Wakili: Je, una kumbukumbu ya barua aliyoiandika Balozi Mahalu kuhusu kusaini mkataba wa pili?
Shahidi: Sikumbuki.
Wakili: Je, una kumbukumbu ya kauli ya serikali iliyoitoa bungeni katika kikao cha 39, Agosti 3, mwaka 2004?
Shahidi: Sikumbuki (akapewa hansard ya Bunge kuhusu suala hilo).
Baada ya kuisoma hansard hiyo, shahidi huyo alikiri kuwa serikali ilikuwa imenunua jengo hilo kwa sh bilioni tatu na taratibu zote za manunuzi zilifuatwa.
Katika kesi hiyo, Balozi Mahalu na Ofisa Ubalozi, Grace Martin, wanadaiwa kula njama na kuisababishia Serikali ya Tanzania hasara ya euro 3,098,741.40.
Kesi imeahirishwa hadi Machi 14, mwaka huu, itakapoendelea kusikizwa.

