Lowassa: Tutajieni mafisadi
November 26, 2007
WAZIRI Mkuu, Edward Lowassa, amekana serikali kuwatambua watu wanaotajwa kuwa vigogo wake, wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya na rushwa.
Kwa kuwa serikali haiwatambui watu hao, Lowassa amewataka watu, wakiwemo viongozi wa dini na katika sekta mbalimbali nchini, kuwataja vigogo hao ili serikali iwashughulikie.
“Nasema watajeni, na ninaahidi tutawashughulikia bila kujali cheo cha mtu au nafasi aliyonayo katika taifa hili na nje ya taifa,” alisema Lowassa.
Alisema hayo jana alipokuwa akihutubia waumini na watu mbalimbali waliofika kwenye viwanja vya Kanisa ka Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Bungo mjini hapa, katika sherehe za kumuweka wakfu Askofu wa kanisa hilo Dayosisi ya Morogoro, Jacob ole Mameo.
“Jamani kwa muda mrefu nimekuwa nasikia wanaokamatwa kwa dawa za kulevya na rushwa eti ni watu wadogo wadogo huku vigogo wakitazamwa, tatizo ni kuwa mnasema tu vigogo, vigogo hamuwataji,” alisema Lowassa.
Waziri Mkuu aliwasihi waumini wa dini zote kuisaidia serikali katika vita dhidi ya rushwa na dawa za kulevya baada ya maelezo yaliyotolewa na Askofu Mameo, kuwa bila ushirikiano vita hiyo haitakwisha.
Katika hotuba hiyo, Lowassa, aliutaka uongozi wa Mkoa wa Morogoro kusimamia vema haki za wananchi katika migogoro ya ardhi inayowakabili kwa muda mrefu, ili kuepusha matatizo yayoweza kujitokeza.
“Mimi niendelee kuwaomba viongozi hasa wa dini kuisaidia serikali katika mapambano haya na matatizo ya ardhi ambayo ufumbuzi wake unahitaji busara kutoka kwenu,” alifafanua.
Baada ya kusimikwa rasmi kuliongoza kanisa hilo, Askofu Mameo alisema dayosisi ya Morogoro imekuwa msitari wa mbele kuisaidia serikali kuboresha huduma za jamii zikiwemo elimu, maji na afya.
“Hadi sasa tangu ianzishwe, dayosisi hii tumefanikiwa kuboresha mambo mbalimbali ikiwemo kuchimba visima 22 vya maji safi kwenye wilaya, kata na vijiji,” alisema Askofu Mameo.
Aidha, alisema kanisa hilo liko msitari wa mbele katika mapambno dhidi ya ujambazi, dawa za kulevya, rushwa na mimba kwa wanafunzi.
“Kuna usemi usemao kelele za chura hazimzuii ng’ombe kunywa maji mtoni, usemi huu hasa ni kichocheo cha watu kuendelea kushiriki katika vitendo hivyo bila woga… serikali iongeze nguvu,” alisema askofu huyo.
Kuhusu migogoro ya ardhi mkoani hapa, alifafanua kuwa itakuwa chanzo cha kuvunja ndoto za maisha bora kwa kila Mtanzania, iwapo juhudi za makusudi hazitachukuliwa kunusuru tatizo hilo, lililoota mizizi katika jamii ya wakulima na wafugaji.
Naye Askofu Mkuu wa kanisa hilo nchini, Alex Malasusa, aliyemweka wakfu askofu huyo, alimhakikishia Waziri Mkuu kwamba, KKKT itaendelea kuwashauri wananchi katika masuala ya amani, maendeleo na kukuza uchumi.
Kusimikwa kwa askofu Mameo, kunafungua ukurasa mpya wa kanisa hilo kuwa askofu wa pili baada ya aliyekuwepo, Askofu Richard Kitale, kumaliza muda wake kwa mujibu wa katiba ya kanisa hilo.
Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima

