Kili Stars kujifua U/Taifa leo

November 18, 2007

BAADA ya kujifua kwa wiki moja katika machimbo ya Bulyanhulu, timu ya soka ya taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, leo itashuka katika dimba la Uwanja wa Taifa wa zamani, jijini Dar es Salaam kwa mechi maalum.

Ni mechi maalumu kwani kitakachofanyika ni wachezaji wa timu hiyo kujigawa sehemu mbili, lengo ikiwa ni kocha wa timu hiyo, Mbrazil, Marcio Maximo kutaka kuona ni kiasi gani vijana wake wameelewa mafunzo.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), Florian Kaijage alisema jana, mechi hiyo itahusisha wachezaji wa timu hiyo pekee na kusema itakuwa haina kiingilio.

“Kocha Maximo ameamua kuandaa mechi hii ili kuwapima vijana wake baada ya mazoezi ya siku kadhaa katika kujiandaa na Kombe la Chalenji,” alisema Kaijage na kuongeza:

“Ingawa ni mechi ya wao kwa wao, ni mechi itakayokuwa na ushindani mkubwa kwani kila mchezaji atalazimika kuonyesha uwezo wake ili kumshawishi kocha kwamba anastahili kubaki kikosini,” alisema Kaijage.

Kwa mujibu wa Kaijage, Maximo amewataka wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake, kujitokeza kwa wingi kushuhudia mechi hiyo ili kuongeza hamasa kwa wachezaji wa timu hiyo.

Alisema kwa kutambua umuhimu wa mechi hiyo, TFF imeamua watazamaji wataingia bure na kwamba, itaanza saa 10 jioni.

Stars iliyo kundi A, imepangwa kufungua dimba katika Kombe la Chalenji na jirani zao Kenya, Harambe Stars mechi itakayopigwa Desemba 8, kwenye uwanja huo.