Kikwete alidanganywa Misungwi
October 29, 2007
IMEELEZWA kuwa uongozi wa Hospitali ya Wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza, ulimdanganya Rais Jakaya Kikwete kuwepo kwa chombo cha X-ray hospitalini hapo, Tanzania Daima imebaini. Wakati wa ziara yake ya mwezi Mei mkoani humu, Rais Kikwete alifika katika hospitali hiyo na wakati akiweka jiwe la msingi katika jengo la X-ray, alionyeshwa mashine hiyo kwa madai kuwa ndiyo itakayokuwa ikifanya kazi.
Hata hivyo, inadaiwa kuwa mashine hiyo iliazimwa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC) ya jijini Mwanza na ilitumika kama hadaa kwa Rais Kikwete.
Siri hiyo ilibainika wilayani humo mwishoni mwa wiki iliyopita, baada ya wananchi wa wilaya hiyo kuubana mbavu uongozi wa hospitali hiyo wakitaka kuelezwa kilipo chombo hicho cha X-ray, baada ya wao kuikosa huduma hiyo tangu jengo hilo liwekewe jiwe la msingi.
Wananchi hao walitaka ufafanuzi na maelezo ya kina kwa nini hawapati huduma hiyo wakati Rais Kikwete alionyeshwa mashine ya X-ray wakati alipoweka jiwe la msingi.
Mmoja wa wananchi hao, aliyejitambulisha kwa jina la Masalu Shaaban aliuliza: “Ni kwa nini X-ray aliyoonyeshwa Rais Kikwete siku hizi haionekani hospitalini? Imepelekwa wapi na uongozi?”
Kufuatia swali hilo, lililoulizwa mbele ya Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Mkuu wa wilaya hiyo ya Misungwi, Magalula Said Magalula, Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Boniventura Bisulu, alisema X-ray hiyo waliiazima katika Hospitali ya Bugando kwa ajili ya kumuonyesha na kukwepa aibu kwa Rais Kikwete.
“X-ray tuliyokuwa nayo tulipewa na uongozi wa Hospitali ya Mkoa (Sekou-Toure), na hiyo tuliyoionyesha kwa rais tuliiazima Bugando ili katika ufunguzi wa jengo hilo ionekane kweli tuna chombo hicho”, alidai Dk. Bisulu.
Mganga Mkuu huyo aliyekiri mbele ya kaimu mkuu wa mkoa, aliridhia pia malalamiko yote yaliyoelekezwa katika hospitali yake hiyo, na kusema kuwa wanafanya jitihada kuondoa adha ya ukosefu wa chombo hicho cha kupimia wagonjwa.
Wananchi hao waliohudhuria kwenye mjadala wa mapambano dhidi ya rushwa katika sekta ya afya, ulioandaliwa na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa nchini TAKUKURU), waliutupia lawama nzito uongozi wa hospitali hiyo na kudai kuwa haufai.
Hata hivyo, juhudi za kuupata uongozi wa Hospitali ya Bugando ili kueleza ni kwa nini waliiazimisha X-ray hiyo kwa hospitali nyingine, hazikuweza kuzaa matunda.
Katika ziara hiyo hospitalini hapo, Rais Kikwete alielezea kufurahishwa na jitihada zilizofanywa na uongozi wa hospitali na wilaya hiyo kwa ujumla kwa kupata chombo hicho muhimu katika tiba.

