Kikwete aenda Kenya

February 27, 2008

MWENYEKITI mpya wa Umoja wa Afrika, Rais Jakaya Kikwete, ameondoka nchini jana kwenda Nairobi, Kenya kuendeleza juhudi za kusaka suluhu kutokana na mgogoro wa kisiasa unaoikabili nchini hiyo. Rais Kikwete anakwenda kusaidia juhudi hizo Kenya wakati pande zinazovutana zikiwa katika mabishano makubwa kuhusu njia muafaka ya kumaliza tofauti zao.

Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Habari wa Ikulu, Salvatory Rweyemamu, ilisema kuwa Rais Kikwete amekwenda Kenya baada ya kuombwa na pande mbalimbali zinazohusika na mgororo huo. Pia ameombwa na mpatanishi katika mgogoro huo wa kisiasa na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Dk. Kofi Annan.

Kwa mujibu wa Rweyemamu, katika ziara hiyo ya siku mbili, Kikwete atakutana na kufanya mazungumzo na Dk. Annan, Rais Mwai Kibaki na kiongozi wa Chama kikuu cha upinzani cha ODM, Raila Odinga.

Kwa muda sasa Dk. Annan amekuwa akiongoza juhudi za upatanishi katika mgororo wa kisiasa nchini Kenya kwa niaba ya Umoja wa Afrika (AU). Katika kazi hiyo anashirikiana na Rais mstaafu Benjamin Mkapa, na Graca Machel, ambaye ni mke wa Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela.

Mgogoro wa kisiasa nchini Kenya ulizuka mwishoni mwa mwaka uliopita baada ya ODM kuyakataa matokeo ya kura za urais kulingana na matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi nchini humo (ECK) yaliyompa ushindi Kibaki.

ODM wanaamini kuwa, chama chao kiliporwa ushindi kwa hila na kuamsha vurugu zilizosababisha kuuawa kwa mamia ya watu na maelfu wengine kuyakimbia makazi yao. Rais Kikwete anatarajiwa kurejea leo.


Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post
 |  TrackBack URI for this post

Comments

Got something to say?