Kaseba Bingwa wa Dunia
November 26, 2007
BONDIA Japhet Kaseba wa Tanzania, juzi usiku alitwaa ubingwa wa dunia wa mchezo wa kickboxing, baada ya kumnyuka Abhijeet Pektar wa India, hivyo kumvua taji hilo katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
Kaseba anayeshikilia pia ubingwa wa Tanzania na Mabara, alitwaa taji hilo baada ya kumaliza kazi katika dakika ya pili na sekunde ya 27 ya raundi ya kwanza ya pambano hilo la raundi tano.
Pektar, ndiye alikuwa wa kwanza kufanya mashambulizi matatu, ingawa moja ndilo lililompata Kaseba. Hata hivyo, Kaseba alipoanza kulipa kisasi, ndiyo ukawa mwisho wa pambano.
Akizungumza baada ya pambano hilo, Kaseba alisema ni faraja kubwa kwake na Tanzania kwa sababu ametimiza ndoto ya siku moja kutwaa ubingwa wa dunia.
“Nafurahi nimetimiza ndoto yangu ya kuwa bingwa wa dunia, hii ni zawadi kwa Watanzania wote, ambao wamekuwa wakiniunga mkono siku zote,” alisema Kaseba.
Kabla ya mpambano huo ulioandaliwa na Shirikisho la Masumbwi Tanzania (PST), kulikuwa na mapambano kadhaa ya utangulizi, ya kickboxing na ngumi za kawaida.
Katika kickboxing, Salum Omari alimnyuka kwa KO raundi ya pili, Dragon Kaizu, Hassan Dragon akamshinda kwa pointi Hamisi Mwaitai na Said Kuchi akamtandika Mohammed Chinga kwa KO raundi ya tatu, wote uzani wa light.
Shukuru Samata, alimtwanga Khalid Manji kwa KO katika raundi ya pili, Hamisi Mwakinyo alimshinda Masudi Mkalambati kwa KO, raundi ya kwanza.
Naye Golota Moses akatoka sare na Said Jeba na Ally Mbutike akamshinda Amira Rajab kwa TKO raundi ya kwanza.
Katika masumbwi, Malik Kinyogoli alimtuliza Venance Mponji kwa TKO huku Hassan Matumla akimshinda kwa pointi Kalama Nyilawila katika uzani wa middle.
Deo Njiku akamnyuka Hussein Pazzi kwa TKO katika raundi ya pili katika kuwania ubingwa wa taifa uzani wa light walter.
Hata hivyo, mshindi hakupewa mkanda kwa madai alizidi uzito, hivyo kuzusha vurugu kwa wengi kuhoji kama hivyo ndivyo, pambano lilikuwa na maana gani.
Malalamiko mengine yalikuwa katika pambano la Ashraf Suleiman na Joseph Marwa, kwa wengi kukerwa na maamuzi, kwani licha ya Ashraf kushindwa kuendelea na mchezo kwa kujeruhiwa, ndiye alitangazwa mshindi.
Imeanidkwa na Ruhazi Ruhazi wa gazeti la Tanzania Daima

