JK: Miaka miwili nyuma
December 21, 2007
Desemba mwaka 2005 siku chache tu kabla hajaingia madarakani, Rais Jakaya Kikwete wakati huo akiwa mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) alifanya mahojiano ya ana kwa ana na Absalom Kibanda ambaye sasa ni Mhariri Mkuu wa gazeti hili. Mahojiano hayo yalichapishwa katika gazeti la Mwananchi Jumapili. Haya ndiyo mambo ambayo alizungumza akitoa mwelekeo wa namna atakavyoongoza nchi iwapo angeshinda uchaguzi na kuwa Rais wa Nne wa Tanzania. Mwandishi: Umejifunza nini tangu ulipoteuliwa rasmi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa mgombea urais.
Kikwete: Inategemea ni jambo gani ambalo ninyi mngetaka niwaeleze. Kwanza ni kwamba nimegundua ni suala linalohitaji kujitoa sana, hasa katika muda unaotumia, lakini pia kwa upande wa nguvu, kwa kweli unapaswa kuwa na afya njema ili uweze kukabiliana na changamoto zilizo mbele yako.
Nimesafiri nchi nzima kwa njia ya barabara, njia ambazo ni ngumu na mbaya. Lakini pia ni kazi ngumu hasa kutokana na idadi kubwa ya mikutano unayopaswa kuhutubia. Unapopita barabarani unakutana na makundi ya watu wanaokutakia mema, wanaotaka wakuone. Kwa kweli ni uzoefu wa aina yake, ingawa ni uzoefu wenye matunda mema. Nimepata fursa ya kuiona nchi nzima na kutambua changamoto zilizo mbele yangu.
Mwandishi: Ni mtu gani ambaye ndiye aliyekujenga?
Kikwete: Mtu aliyenijenga kwa namna gani sijui?
Mwandishi: Kisiasa.
Kikwete: Kisiasa mtu wa namna hiyo kwangu ni Julius Nyerere. Kwa sababu … Nilipoanza kujenga mapenzi katika siasa yeye ndiye aliyekuwa baba wa siasa hapa, maisha ya kisiasa yalihusishwa na yeye. Kwa hiyo yeye ndiye naweza kusema ndiye msingi wa maisha yangu ya kisiasa.
Mwandishi: Unaonekana kujitofautisha na wanasiasa wengine wa kariba yako kimaisha. Hivi karibuni kwa mfano, mtoto wako mkubwa wa kiume (Ridhwan) alihitimu shahada ya kwanza ya sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kabla ya hapo alipata elimu ya sekondari hapa hapa akianzia Shaaban Robert na baadaye Sekondari ya Mkwawa. Je, ni mkakati wako mahususi au ni tukio la bahati tu?
Kikwete: Inategemea hasa uwezo wa mtu kulipa gharama za elimu nje ya nchi ambako ni ghali sana. Ninakumbuka kwamba alipata nafasi ya masomo Uingereza, katika chuo cha Oxford nikashindwa kumpeleka kule kwa sababu ya ukubwa wa gharama ambazo sikuweza kuzimudu. Sasa unafanya nini katika hali hiyo!
Mimi ninaamini kwamba elimu inayotolewa katika nchi hii ni nzuri kama inayotolewa sehemu nyingine duniani. Kitivo cha Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kina hadhi na sifa ya kuzalisha wanasheria makini na wenye uwezo, wanaoweza kufanya kazi sehemu yoyote ndani na nje ya nchi. Kwangu mimi hilo halina shida.
Hivi sasa dada yake Ridhwani anasomea masuala ya tiba katika Chuo Kikuu cha Muhimbili na ninaamini Muhimbili ni chuo kizuri kabisa cha masuala hayo ya tiba. Kwa hiyo niliona hakuna sababu ya kuwasomesha nje iwapo suala ni elimu ambayo wangeweza kuipata hapa.
Mwandishi: Umemtaja Mwalimu kama kiongozi wa mfano kwako, lakini wakati fulani aliwahi kusema kwamba unapokuwa kiongozi wa kisiasa unapata wakati mgumu katika kutenganisha mambo yako ya kifamilia na ya kisiasa na kiserikali. Je, wewe umeweza vipi kuitazama familia yako sambamba na kuendesha shughuli za kiuongozi, unadhani ulitimiza wajibu wako kama mzazi?
Kikwete: Kwa hakika nilitimiza wajibu wangu, lakini nadhani ni bahati kwa hao pia kwani ninaye mtoto mwingine ambaye ni mtukutu, na kwa kweli ninafanya juhudi kubwa kwake. Ingawa ndiye aliye na akili kati ya watoto wangu wote, anaonyesha kutokuwa na hamu ya kujiendeleza kielimu. Inategemea bahati, kwani katika maisha, moja jumlisha moja haiwezi kuwa mbili. Hata hivyo ninafarijika sana kwamba Ridhwani na dada yake wamefikia hapo.
Mwandishi: Iwapo utafanikiwa kuwa rais katika nchi maskini kama hii, unadhani utapata fursa ya kuendelea kuwaangalia vyema watoto wako?
Kikwete: Hebu nisubiri nione namna ninakavyogawa muda wangu. Ninafanya kila ninaloweza kwani ni wajibu wangu kuhakikisha kwamba watoto wangu wanafanikiwa katika maisha.
Mwandishi: Kuna hili suala la kuchangia elimu na afya ambalo limekuwa likilalamikiwa kwamba limeshindwa kuzaa matunda mema. Je, ukiwa rais unao mpango wowote wa kuliangalia suala hili?
Kikwete: Kwa hakika sina majibu katika kila swali kwa wakati huu. Unatakiwa kufika kwanza huko ili ujue nini kifanyike. Uamuzi wa kuchangia baadhi ya huduma ulifikiwa kwa kuzingatia hali halisi. Mwanzoni serikali ilifikiri ingeweza kugharamia kila kitu lakini mwishoni ikaonekana kwamba huduma nyingi zilizorota. Jambo muhimu hapa ni kujenga na kuendelea kudumu.
Ni kiasi gani watu watachangia, ni kiasi gani kitachangwa na serikali, siwezi kuwa na jibu la moja kwa moja hivi sasa, ingawa nina uhakika nitakapoingia madarakani nitaliangalia jambo hilo. Hata hivyo mimi ninaona watu wanapaswa waweze kumudu elimu, waweze kupata huduma za afya, waweze kupata maji….Kuhusu nini kifanyike iwapo watu watashindwa kumudu, ni lazima uhakikishe kwamba hakuna mtu anayeshindwa kumudu kwa sababu ya umasikini wake au uzee. Ninachoweza kusema ni kwamba, hebu tusubiri nifike kule tuone nini tutafanya, kwani siko tayari kuona watu wakishindwa kupata huduma hizo.
Mwandishi: Kumekuwa na hoja kwamba, pengo kati ya matajiri na maskini limekuwa likiongezeka na wakati fulani hata Mwalimu Nyerere aliwahi kutahadharisha kuhusu jambo hilo. Wewe unalitazamaje jambo hilo?
Kikwete: Kwa kweli pengo linaongezeka, ni jambo dhahiri, kwangu naona changamoto ni kuwaangalia hawa maskini wanavyoweza kusaidiwa kuondoka huko. Hiyo ndiyo changamoto. Wakati mwingine huwa naona hili lazima litazamwe kwani hatuwezi kugawana umaskini. Pengo lipo kweli, ingawa hawa wanaoonekana kuwa matajiri pia, wanaonekana hivyo kwa sababu tu ya ulinganisho unaofanywa kwa kuwaangalia na maskini waliopo. Kila mara nimekuwa nikisema kwamba, tunapaswa kuchukua hatua za kulitatua hili na kuiondoa nchi yetu katika umaskini.
Mwandishi: Tunaweza kufanyaje basi kukabiliana na utegemezi wa mataifa ya nje?
Kikwete: Ni kweli tumepiga hatua katika hilo katika bajeti kwa mfano kutoka asilimia 80 ya utegemezi hadi kufikia 41. Tunapaswa tuendelee ili tuukabili utegemezi kwa kiwango kikubwa zaidi. Mosi, tunapaswa kufanya kazi zaidi ili uchumi wetu ukue. Tutapaswa kuimarisha makusanyo ya serikali, wigo wa ulipaji kodi inabidi kupanuliwa ili uchumi ukue haraka na kuongeza ajira. Tutaunda serikali ya kufanya hayo.
Mwandishi: Unazungumzia uundwaji wa serikali itakayowajibika. Je, umepanga kufanya mabadiliko katika muundo wa Baraza la Mawaziri si katika idadi tu bali katika muundo wake, pengine kwa kuongeza au kupunguza wizara na tofauti na ilivyo katika serikali ya Rais Mkapa?
Kikwete: Kwa kweli kutakuwa na mabadiliko katika muundo wa serikali, bado hatujafikia tamati katika kulipanga hilo. Ninataka kuwa na serikali inayokidhi mahitaji, kuna mambo ambayo ni muhimu kwangu kama kuwa na serikali inayosikiliza.
Mwandishi: Kwa hiyo unazungumzia aina ya serikali ya askari wa miamvuli?
Kikwete: Ni kweli nahitaji kuwa na mawaziri wenye uwezo wa kutenda. Kwa kweli kuna mambo ambayo kwangu ni muhimu, watu wenye kuheshimika. Jambo moja ni kwamba tunataka kuwa na uhakika wa makuzi ya uchumi, msisitizo wetu mkubwa utakuwa katika uchumi. Tumeshafanya siasa nyingi sasa, na tunataka tulenge katika uchumi.
Tumefanya sana siasa, sasa ni wakati wa kuangalia mustakabali wa kiuchumi namna ya kukabiliana na umaskini, kukuza uchumi, kuongeza ajira. Mtazamo ni kukabiliana na umaskini. Nataka kuwa na serikali ambayo itaziangalia changamoto hizo.
Mwandishi: Umesema utafanya mabadiliko ya kimuundo katika serikali yako. Kwa kuangalia serikali utakayoiunda je, pengine kuna eneo ambalo linahitaji kuundiwa wizara mpya ambayo hivi sasa haipo?
Kikwete: Ni mapema sana kulisemea hilo.
Mwandishi: Je, serikali yako itakuwa na ukubwa gani hasa?
Kikwete: Nadhani ukubwa wa baraza la mawaziri utatokana na mahitaji. Siwezi kusema iwapo litakuwa dogo au kubwa. Hata hivyo nitaunda baraza ambalo nitaweza kulimudu, kwa sababu kuna mambo ambayo ninataka kuyatekeleza kama vile masuala yanayohusu ajira, kilimo, maendeleo, mazingira na maji.
Nimeshasema huko nyuma kwamba suala la maji linanigusa sana. Ninaweza nikaiona hatari ya kuibuka kwa mgogoro mkubwa katika rasilimali maji hapa nchini katika kipindi cha miaka 10 au 15 ijayo hivyo ni lazima tuchukue hatua kuzuia hilo lisitokee.
Mwandishi: Programu nyingine zinazoendeshwa hapa nchini kama zile za MMEM na MMES zinadaiwa kuandaliwa Washington, Marekani. Iwapo hivyo ndivyo utafanya nini katika hilo?
Kikwete: Sina uhakika kama kuna usahihi kudai kwamba programu zetu zinaandaliwa Washington. Hizo zote ni programu tulizoandaa wenyewe ingawa mfadhili wake mkuu ni Benki ya Dunia. Ni kama vile tunapoandaa ujenzi wa mtandao wa barabara za Afrika Mashariki, nchi hizi tatu za Afrika Mashariki zilikaa pamoja tukawa tukitafuta kuungwa mkono na wahisani, na tukatafuta atakayewashawishi wahisani hao na Umoja wa Ulaya wakafadhili na mimi nilikwenda huko tukajadili wakaahidi kupeleka hoja yetu katika mkutano wa wahisani na walipolipeleka suala hili na Benki ya Dunia nayo ikaingia kusaidia. Tunahitaji mtandao mmoja wa barabara Afrika Mashariki, tunataka kuwa na soko la pamoja, tunataka kujenga soko linalotegemeana, na katika hilo unahitaji mawasiliano. Kwa hiyo ninachosema ni kwamba mahitaji yetu hayaanzii kwa wahisani.
Tunajua shule za msingi zikipanuka tunapaswa kuendeleza elimu ya sekondari. Kuna mambo tunaweza kufanya wenyewe, ingawa tunahitaji pia msaada wa wahisani. Katika misingi hiyo tunapaswa kuwasiliana na taasisi ambazo zikiwasiliana na wahisani watasikiliza.
Ni kama vile IMF wanaposema Tanzania ni nzuri, si kwamba IMF wanatoa hela nyingi, tunachohitaji kutoka IMF ni kauli tu kwamba, mnaweza mkafanya biashara na Tanzania. Unapaswa kuukubali ukweli huu wa mahusiano ya kilimwengu. Kwa hiyo programu hizo zimeanzishwa hapa hapa nyumbani, ingawa zikapata ufadhili mkubwa wa wahisani.
Mwandishi: Tumeyaona mafanikio shule za msingi na hata sekondari. Nini unategemea kufanya kuendeleza elimu ya juu?
Kikwete: Sawa, sawa kabisa, nimekuwa nikilizungumzia hili, kuhusu elimu ya juu kwa sababu ni kweli kwamba idadi ya wanafunzi wanaojiunga na shule za msingi ni kubwa, tunahitaji kupanua elimu ya sekondari, na tukiwa na ongezeko kubwa la wanaojiunga na elimu ya sekondari tutapaswa kupanua elimu ya juu. Na kila nilikopita nimekuwa nikilisema hili. Kwa mfano mwaka huu watu waliopata daraja la kwanza Kidato cha Sita wameshindwa kujiunga chuo kikuu kwa sababu ya uhaba wa nafasi.
Kwa kweli tunapaswa kupanua elimu yetu. Kwanza tunatakiwa kupanua vyuo vikuu tulivyonavyo sasa ili watoto wengi wapate nafasi ya kusoma, hilo nalo linahitaji mambo mengine yafanyike, kuwe na madarasa zaidi, vyumba vya kuhadhiri, maabara nyingi, walimu wengi zaidi, makazi zaidi ya wanafunzi.
Na hayo ni baaadhi ya matatizo yanayokikabili Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wameongeza idadi ya wanafunzi isiyolingana na miundombinu.
Hatuwezi kupuuzia wajibu wa kujenga chuo kikuu kingine. Tunapaswa kuangalia uwezekano wa kujenga chuo kikuu kingine, kikubwa zaidi ambacho kitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi wengi zaidi. Tumekuwa katika baadhi ya nchi ambako wanafunzi 40,000 wanasoma chuo kimoja.
Mwandishi: Chuo hiki kitajengwa Dodoma, Mwanza au wapi?
Kikwete: Hapana, hapana sijui ni wapi lakini hakiwezi tena kuwa Dar es Salaam.
Mwandishi: Hata hivyo kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa watu kuhusu miradi kadhaa ambayo serikali imeifanya na si tu malalamiko….
Kikwete: Mradi kama upi kwa mfano?
Mwandishi: Kama ule wa IPTL ambao umelalamikiwa sana. Ukichaguliwa kuwa rais utafanya nini ili kuepukana na makosa ya namna hiyo tena?
Kikwete: Ninadhani kuna mambo tuliyofanya huko nyuma ambayo yanapaswa kusahihishwa, siwezi kusema kwamba nitaingia katika serikali na kuifanya kazi yangu ya kwanza kuwa ni kutafuta makosa. Hilo litakuwa na matokeo mabaya, utaishia kuibua hisia zisizo za lazima katika jamii, na mwisho watu watakuanaje sijui.
Ninachosema, changamoto yetu ni kuona tunatimiza wajibu, mambo yanasonga mbele vizuri, katika maeneo ambayo mambo hayakwenda sawa yaanze kutengemaa. Nadhani hiyo ndiyo nia yetu.
Mwandishi: Lakini kumekuwa na madai ya kukuhusisha na hili suala la IPTL kwamba lilijadiliwa ukiwa waziri pale (Wizara ya Maji, Nishati na Madini) na likasainiwa wakati ukiwa Waziri wa Fedha, je, ni kweli unahusika?
Kikwete: Si kweli, si kweli, nendeni mkatazame vizuri ukweli ulivyo, huo ni mkataba ambao ulisainiwa kati ya Mei na Juni 1995 wakati mimi niliondoka Nishati mwezi Novemba 1994. Dhamira yangu ni pevu kabisa kwamba sikuhusika kabisa katika majadiliano.
Kuna mambo mawili katika jambo hilo. La kwanza ni lile linalohusu uamuzi wa kuruhusu wazalishaji wengine wa umeme kuingia nchini mbali ya Tanesco. Huo ndiyo uamuzi ambao mimi niliuchukua, niliruhusu IPTL na nikaruhusu Songas kuingia. Jambo la pili ni lile la mkataba wa mgawanyo wa nishati itayozalishwa (Power Sharing Agreement), ambao Tanesco ilifanya majadiliano na wazalishaji wa umeme. Sikushiriki katika kufikiwa kwa mkataba huo wa mgawanyo kati ya Songas na Tanesco, na sikushiriki katika mkataba wa mgawanyo kati ya Tanesco na IPTL.
Mwandishi: Kwa hiyo unasema hukuhusika katika mkataba wa IPTL na Tanesco?
Kikwete: Ndiyo kuna mambo mawili hapo, sehemu yangu mimi ilikuwa ni ile ya kisera kwani kabla ya hapo ni Tanesco tu waliokuwa na jukumu la kuzalisha umeme. Uamuzi niliochukua ulikuwa ni wa kuruhusu wadau wengine kuingia na kuzalisha umeme. Lakini wazalishaji hawa wengine baada ya kuzalisha umeme wanapaswa kuuza kwa Tanesco. Mkataba wa ununuzi wa nishati, yaani Tanesco kununua umeme kutoka IPTL, Tanesco kununua umeme kutoka Songas. Suala lenye matatizo hapa ni hili la mkataba wa ununuzi wa umeme. Na mkataba huu haukusainiwa mimi nikiwa pale? dhamira yangu iko bayana katika suala hili.
Mwandishi: Ahsante kwa kuliweka wazi suala hili…
Kikwete: Ni kweli jambo lenye utata hapa na ambalo linazua manung’uniko ni hili la mkataba wa mgawanyo wa uzalishaji na kuuziana umeme. Hilo ndilo linaloonekana kuwa tatizo hapo. Mimi la kwangu ni la kuruhusu IPTL na Songas waje hapa… Sioni ni kwa nini nilaumiwe kwa hilo, leo hii hakuna uzalishaji wa umeme kutokana na kukosekana kwa maji katika Bwawa la Mtera.
Mwandishi: Kwa hiyo unasema ulikuwa ni uamuzi sahihi?
Kikwete: Ndiyo! Hilo uamuzi wangu ule hauna kasoro hata kidogo?
Mwandishi: Kwa sababu hiyo basi haya ni matunda ya maamuzi yako?
Kikwete: Ndiyo, ninajua hilo kwa kuwa iwapo nisingeruhusu IPTL, Songas basi leo hii tusingekuwa na umeme kabisa katika nchi hii, kwani tulikuwa tukitegemea umeme wa kuzalishwa kwa maji ambayo hivi sasa yanakatisha tamaa. Shida hapa ni ule mkataba wa kuuziana umeme ambao mimi sikushiriki katika mjadala wake.
Mwandishi: Turejee kwa upande wa kampeni. Ni nani anafadhili kampeni zenu?
Kikwete: Nilichozungumza Songea ni kwamba malakamiko kuhusu vitendo vya rushwa katika uteuzi wa wagombea vinapaswa kutafutiwa ufumbuzi. Kumekuwa na malalamiko kwamba katika uteuzi kuna fedha nyingi zinatumika. Ni jambo tunalopaswa kulimaliza, kwa kukaa na kulijadili. La kwanza ni mchakato mzima wa uteuzi kutoka udiwani, ubunge hadi urais.
Huko nyuma tuliwahi kufanya mabadiliko baada ya kuwapo kwa malalamiko ya wanasiasa wasio waaminifu waliokuwa wakitumiwa mwanya wa kutoa rushwa katika mfumo ule wa zamani wa uteuzi uliokuwa ukifanywa katika ngazi ya wilaya. Hayo ni mambo ambayo tunapaswa kuyaangalia.
Hivyo baadaye tukaamua kuwa na mkutano wa jimbo. Bado kukawa na malalamiko. Wanasiasa wajanja, wenye hila wanaweza kuwanunua kundi kubwa la wapigakura. Tatizo bado liko na linatakiwa kupatiwa ufumbuzi.
Mwandishi: Je, unakiona chama kikiwa kimegawanyika?
Kikwete: Hapana. Yapo maeneo ambako imewachukua muda mrefu watu kupona majeraha, wengine wanachukua mambo haya kama ya kawaida wakati wengine wanayaona kuwa makubwa. Hilo ndilo linalowafanya wengine waone kuwa kuna mgawanyiko ndani ya chama wakati kilichomo ni makundi tu. Tunapaswa kukabiliana na tatizo la rushwa, si ndani ya chama tu bali pia hata katika uchaguzi mzima kitaifa.
Suala moja ni dhahiri kwamba huwezi kupinga matumizi ya fedha. Unahitaji fedha katika kampeni, unatakiwa kusafiri, unahitaji mafuta. Suala ni namna gani tunapata fedha hizo. Je, ni fedha safi? Ni lazima tuwaepuke watu wanaochangia na kuishia kuwafanya wabunge waliochaguliwa wakiwa mateka wao kisiasa. Naona tunapaswa kuwa na taratibu zinazoeleweka katika kujua fedha za kuendesha kampeni.
Mwandishi: Ukiangalia mchakato mzima wa namna ulivyopitishwa na chama chako na kuwa mgombea urais, unadhani wewe hauko katika hatari ya kuwa mateka wa watu wa namna hiyo?
Kikwete: Sintakuwa, sintakuwa. Jambo zuri katika mfumo niliopo mimi ni kwamba mosi nimepewa maelekezo ya kujiweka kando ya utaratibu mzima wa upatikanaji wa fedha za kampeni kwa hiyo hakuna mfadhili ambaye anakutana na mimi moja kwa moja na ambaye nikifanikiwa kuingia ikulu akaja kwangu ikulu akasema, mzee unajua nina shida ninajua nilikusaidia sana.
Tumeunda kamati ya kitaifa ya kampeni yenye jukumu la kufanya hivyo. Yeyote anayekuja kwangu na kutaka kutoa fedha ninamwambia hapana, usizungumze na mimi na nenda kwa Katibu Mkuu ili kuepuka mtu kuja kwangu na kuniambia, Mzee unajua tulihangaika! kontena yangu imekwama bandarini (kicheko)…
Mwandishi: Je, ukichaguliwa kuwa rais utahamishia makao makuu ya serikali Dodoma?
Kikwete: Mimi nadhani sina mpango wa kufuta mpango wa kuifanya Dodoma Makao Makuu ya Serikali. Unapokuwa nje ya serikali huwezi kusema mengi, na unatakiwa kusubiri hadi utakapoingia. Tunapaswa kupanga. Kuna wakati nilipokuwa Waziri wa Maji, kulikuwa na mpango wa kuhamishia wizara tano Dodoma. Lakini idadi ya nyumba ikawa pungufu kuliko idadi ya wafanyakazi na pia mahitaji mengine kama shule kwa ajili ya watoto wa wafanyakazi waliokuwa wakizidi 2000 zilikuwa hazitoshelezi.
Ni kitu kinachowezekana, kinachotakiwa ni mipango mizuri na ya uhakika. Miundo mbinu ya kutosha kwa kujua idadi ya majengo kwa ajili ya wafanyakazi, majengo ya wizara. Ni lazima tujue ni wizara gani inapaswa kuhamishwa kwanza hivyo tunatakiwa kujua idadi ya wafanyakazi wa wizara hiyo na familia zao kwa ajili ya shule.
Kama mkiamua kwamba tunataka kuhamisha wizara tatu. Kwa hiyo mkajiuliza nini kinatakiwa kwa ajili ya wizara hizo, ni lazima tujue kama kuna majengo ya kutosha, kuna maji?
Ingawa sasa maji si tatizo Dodoma. kwa hiyo tukipanga kwa namna hiyo tunaweza tukahama hata kama katika ni katika kipindi cha miaka 10 hadi 15, kila mwaka mnaweza mkahama wizara moja moja.
Mwandishi: Hivyo ndivyo utakavyofanya?
Kikwete: Hapana, hapana, ninachosema ngoja nifike nione hili linaweza kufanywa namna gani. Lakini mimi nasema bado ni lazima tuendelee kuifanya Dodoma makao makuu ya serikali tunapaswa tupange sawasawa kuja Dodoma.
Mwandishi: Utafanya nini kuumaliza mgawanyo kule Unguja kati ya Unguja na Pemba na kati ya CCM na CUF?
Kikwete: Mimi nasema hiyo ni moja ya changamoto tulizonazo. Naaa…moja ya kitu tumekuwa tunazungumza na wakubwa hawa, kule Zanzibar wanaona suala ni namna uchaguzi ulivyoendeshwa na kusimamiwa. Lakini safari hii uchaguzi mkuu uliendeshwa vizuri kabisa.
Mwandishi: Uliendeshwa vizuri Pemba tu au hata Unguja?
Kikwete: Aaha! Nasema hivi..tazama…hata kule Unguja ni Mji Mkongwe tu kulikuwa na kelele jamani lakini uchaguzi ulifanyika vizuri. Hata ripoti ya NDI mimi ninayo.
Mwandishi: Lakini inaeleza kuwa watu walionekana wakienda kupiga kura wakati vidole vyao vikiwa na wino unaoonyesha kwamba walishapiga kura.
Kikwete: Hata ile NDI wanasema kuna ripoti zinazoeleza kwamba kuna askari walionekana… unaona! lakini ile sehemu ambayo waliiona wenyewe wanasema vituo vilifunguliwa kwa wakati, vifaa vya kupigia kura vilikuwapo, maafisa wa uchaguzi walifanya shughuli zao vizuri, mawakala wa vyama walikuwapo, wanakuambia mtu yeyote ambaye hakuandikishwa katika kile kituo hakuruhusiwa kupiga kura, Hivyo ndivyo vitu walivyoviona ndiyo. Ila wanasema… ila kosa la wale maafisa ni kwamba hawakuwasaidia wale waliokuwa wakihangaika wapi wakapige kura. Wanaendelea. vituo vilifungwa kwa wakati, kura zilihesabiwa vituoni, waangalizi waliruhisiwa kuona zoezi la uhesabuji, halafu wanasema baada ya kuhesabu kura kila chama kilipewa fomu zake za matokeo. Wanasema ingawaje tumesikia kuna vituo fomu hazikuwepo lakini kwenye vituo vyote tulivyokuwapo fomu zilikuwapo. Sasa nasema hivi iwapo hilo ndilo lililofanyika, sasa kwa hiyo……
Mwandishi: Ni kweli kwamba hata waangalizi wengine kama wa Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Madola waliona kuboreshwa kwa taratibu za uchaguzi kuliko ilivyokuwa mwaka 1995 na 2000. Je, kwa matokeo yale ya Zanzibar kweli CCM inaweza kuendelea kutawala peke yake pasipo CUF?
Kikwete: Aaaha.. hebu tazama, Je, Zanzibar inaweza kuongozwa na vyama mchanganyiko? Je, CCM na CUF wanaweza kuunda serikali makini ya pamoja? Swali hilo jiulize tu? Kwa sababu tunahitaji serikali makini, wanaweza kuchanganyika hawa kwenye serikali moja na kufanya kazi? Mmoja atakuwa anavuta huku na mwingine huku. Ni afadhali mmoja awe kwenye serikali mwingine awe kwenye upinzani. Hizo ndizo fomula tu wanazokuja nazo. Sasa nasema hivi Zanzibar pale suala ni tofauti za kihistoria. Hata ukirudia uchaguzi leo Seif hashindi. Kwa sababu ni hivi, Wapemba watampigia Mpemba na Waunguja watampigia Muunguja na hata kura zile wa Seif ukiziona nyingi Unguja ni za Wapemba. Hata lile jimbo waliloshinda la Mji Mkongwe kaangalie watu wengi pale ni Wapemba. Hii ndiyo Zanzibar, Seif hashindi kwa sababu set-up ya visiwa vile Waunguja ni wengi kuliko Wapemba! Mnaona!
Mwandishi: Je, huoni uamuzi wa CCM wa kumfukuza Seif (Maalim) katika chama umechangia kukua kwa mgawanyiko huu?
Kikwete: Alaa, pengine kama unadhani kuwa alionewa. Sasa kama alifanya uhuni unataka aachwe tu kwa sababu ni Maalim Seif? Ehhee (kicheko). Nimezungumza na wakubwa hawa alikuja mama yule wa Marekani nikamwambia, nashukuru hata Jack Straw aliwanukuu waangalizi, tunachopaswa kuangalia ni namna gani tutakavyowatoa Wazanzibari hawa kwenye tatizo la mgawanyiko wa kihistoria. Usipowatoa pale arrangement ile ngumu sana? Pale tufanye jitihada za kuwaondoa pale Wazanzibari.
Mwandishi: Utauendeleza mwafaka ukiwa rais?
Kikwete: Mwafaka ule utajiendeleza wenyewe, ndiyo msingi …
Mwandishi: Je, utateua mbunge wa CUF kwa mfano kama alivyofanya Mkapa?
Kikwete: Tuangalie huko mbele ya safari….ndiyo… Mimi nasema Zanzibar pale, tuifanye jitihada za kuwaondoa wale Wazanzibari kwenye mgawanyiko wa kihistoria, ndiyo jawabu. mpangilio wowote ule. Mimi nilishasema kule Pemba hatutapata jimbo na wao kama watapata jimbo hata moja Unguja pengine moja kule kwenye maeneo yenye Wapemba.
Mwandishi: Hilo limetokea kwa sababu ya ninyi CCM kuiga utaratibu wa sultani wa kugawa majimbo kule Pemba?
Kikwete: Mimi nasema hivi, hata yale majimbo yangebaki yalivyo matokeo yangebaki yale yale tu kwani kimsingi pale..Kwa bahati mbaya baada ya kurudi kwenye mfumo wa vyama vingi Zanzibar wamerudi kwenye mfumo wao wa migawanyiko ya kihistoria. Ni hayo ndiyo matatizo ambayo lazima tupambane nayo.
Mwandishi: Kwa hiyo unadhani mfumo wa vyama vingine umeshindwa Zanzibar?
Kikwete: Hapana haujashindwa, nasema hizo ni changamoto, watu wamerudi kwenye uhasama wa zamani.
Mwandishi: Sasa tufanyeje?
Kikwete: Hizo ndizo changamoto mbele yetu…ahsante sana
KUTOKA: TANZANIA DAIMA
Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post | TrackBack URI for this post
Comments
Got something to say?

