JK awaonya wanahabari

March 27, 2008

RAIS Jakaya Kikwete amesema dalili mbaya za kuwatumia waandishi wa habari wasiozingatia misingi ya kitaaluma, maarufu kama ‘makanjanja’, inaiweka fani hiyo katika hatari ya kupoteza heshima yake katika jamii.

Kutokana na hali hiyo, Rais Kikwete amewaagiza wamiliki wa vyombo vya habari nchini, wahariri na wanahabari, kuzingatia maadili ya taaluma ya habari ili kuinusuru taaluma hiyo isiangamie kutokana na kuvamiwa na ‘makanjanja’ hao.

Akizungumza wakati wa sherehe za uzinduzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Rais Kikwete alisema iwapo hatua za mara moja hazitachukuliwa mapema, basi wanahabari na wamiliki ndio watakaokuwa watu wa kwanza kujuta, hali itakayosababisha kuanza kusemana wenyewe kwa wenyewe, ambapo dalili zake zimeshaanza.

“Dhamira ya kulinda maadili ya taaluma ya habari inaanzia kwa wamiliki. Mkiacha mtakuwa wa kwanza kujuta na kuanza kusemana na kuchimbana wenyewe. Wamiliki na wahariri msiiache taaluma hii ikachezewa, kwa sababu tunao mwelekeo wa mashaka hivi sasa.

“Mimi naipenda sana taaluma hii, lakini nitawaunga mkono mkizingatia maadili ya taaluma yenu,” alisema Rais Kikwete.

Rais Kikwete alieleza hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa Shirika la Habari Tanzania (TBC), ambalo linaunganisha vyombo viwili vya umma, Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) na iliyokuwa Televisheni ya Taifa (TvT).

Kwa uzinduzi huo uliohudhuriwa pia na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Kapteni George Mkuchika, TBC litakuwa shirika la umma na si idara ya serikali kama ilivyokuwa awali.

Kwa mujibu wa Rais Kikwete, wanahabari wanatakiwa pia kutokuwa waoga wakati wanapoandika habari za ukweli, zisizoegemea upande wowote.

“Chombo cha habari hujijengea heshima kutokana na habari zake za uhakika. Na huu uwe mwongozo na dira ya utendaji kazi katika TBC,” alisema Kikwete.

Katika hatua nyingine, Rais Kikwete aliiagiza menejimenti ya TBC kutoa kipaumbele katika kuwaelimisha na kuwaendeleza watumishi wake, ili waweze kuvitumia vizuri vifaa vya kisasa walivyonavyo na kwenda na wakati.

Aidha, aliviagiza vyombo vyote vya habari nchini kwenda zaidi vijijini na kuandika habari za jamii na maendeleo.

Alisema kuwa, tabia iliyojengeka ya vyombo vya habari kuandika zaidi habari za mijini, si dalili njema kwa maendeleo ya habari na inawanyima haki wakazi wa vijijini ambao ni zaidi ya asilimia 80.

“Tunataka hayo tunayoyasoma na kuyatazama katika luninga na magazeti yetu yahusishe habari za maendeleo vijijini, maana huko kuna habari nyingi za maendeleo na nzuri zaidi,” alisema.

Awali, Mkurugenzi wa TBC, Tido Mhando, alimweleza rais pamoja na wageni waliohudhuria uzinduzi huo kwamba: “Tunataka kuonyesha bayana kuwa tumezaliwa upya kweli kweli, kwa kutangaza vipindi vilivyo bora zaidi na kuondoa vipindi vya zamani, hasa vile vilivyodumu kwa miaka 40.

“Tunataka kufanya mabadiliko makubwa, hasa kwa upande wa redio, na kila mkoa utakuwa na mwakilishi wetu mwenye vifaa vya kisasa.” Mhando alimwakikishia Rais na Watanzania kuwa, dira ya TBC itakuwa ni kukamilishwa kwa mikakati yake kwa kutumia mitambo ya ‘digital’ na kujitegemea kwa asilimia 100 katika kipindi cha miaka mitatu tangu sasa.

“TBC itakuwa fahari kwa kila Mtanzania na tutatoa habari za kweli na za uhakika,” aliahidi.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na wakurugenzi wastaafu karibu wote wa RTD na TvT.