JK amkingia kifua Maximo
December 21, 2007
WAKATI leo Kocha Mkuu wa timu ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Marcio Maximo akiondoka nchini kwenda kwao Brazil kwa mapumziko, Rais Jakaya Kikwete, amemkingia kifua na kueleza kuwa bado ana imani naye na hivyo Watanzania wampe muda na ushirikiano katika jukumu lake la kuijenga Stars. Rais Kikwete alitoa kauli hiyo juzi, wakati wa mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari, katika kutimiza miaka miwili tangu alipoingia madarakani mwaka 2005.
Rais alieleza kushangazwa kwake na baadhi ya wananchi wapenda soka, kuanza kupoteza imani na kocha huyo wakati ana muda mfupi tangu alipoanza kuinoa timu ya soka ya taifa.
“Kuhusu Maximo, inasikitisha, ndiyo, tumetolewa kwenye michuano ya Chalenji, lakini ni mapema mno kumlaumu mwalimu, bado nina imani na Maximo, nina imani na timu ya taifa, tumpe muda, mambo yatakuwa mazuri,” alisema Rais Kikwete.
Hata hivyo, alitoa changamoto kwa wadau wa soka kutambua kuwa wachezaji wa timu ya taifa, hawatokei Taifa Stars, bali kwenye klabu ambako kumetawaliwa na migogoro badala ya kujenga msingi mzuri wa soka.
” Wachezaji wa timu ya taifa hawatokei timu ya taifa, wanatokea kwenye vilabu ambako viongozi wameamua kuwekeza kwenye migogoro, badala ya kujenga msingi mzuri wa soka ili kumwezesha Maximo kuwa na timu bora. Kwa hiyo nawapa changamoto viongozi wa soka, waache migogoro yao, wawekeze kwenye soka, hapo tutafanikiwa…,” alisema na kuongeza:
“Kocha mwenyewe ana mwaka mmoja tu, tayari tunataka timu ianze kufanya maajabu. Tumpe muda, nina imani naye na ataendelea kuwa kocha wa timu ya taifa,” alisema Rais Kikwete.
Kauli ya Rais Kikwete imekuja siku chache baada ya timu ya soka ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, kutolewa katika mashindano ya Chalenji yanayoendelea hapa nchini. Timu ya Taifa ya Zanzibar, ‘Zanzibar Heroes’ nayo imeondoshwa kwenye masindano hayo katika hatua ya robo fainali kwa mikwaju ya penalti.
Hivi karibuni Kocha Maximo alikumbwa na zahama ya kuzomewa na mashabiki, kwa madai kuwa timu hiyo imeonyesha kiwango cha chini na hivyo baadhi ya wadau kuanza kushuku uwezo wake.
KUTOKA: TANZANIA DAIMA
Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post | TrackBack URI for this post
Comments
Got something to say?

