Jimmy Greaves Nguli aliyefanya makubwa England
April 7, 2008
ALIKUWA mmoja wa wafungaji mabao mahiri duniani katika mchezo wa soka kuanzia mwishoni mwa miaka ya 1950 hadi mwanzo wa miaka ya 1970.
Hadi sasa, wengi humkumbuka pale klabu alizochezea au timu ya England zinapotoka uwanjani bila ya kupata mabao.
Hali ikiwa hivyo, utasikia watu wakimtaja Jimmy Greaves, mshambuliaji hatari ambaye safari moja alipoulizwa anapenda nini duniani alisema, chakula, pombe na kupiga mabao dimbani.
Alifunga mabao 44 katika mechi 56 za kimataifa, alizochezea England, mara mbili amefunga mabao manne na mara tatu alitikisa nyavu mara tatu katika mchezo mmoja.
Mpaka sasa, ni mfungaji wa tatu bora katika historia ya Ligi ya England akitanguliwa na Bobby Charlton na Gary Lineker.
Hadi hivi karibuni, alikuwa akichambua habari za soka katika vituo vya televisheni, nchini England.
Alipochezea klabu mbalimbali, Jimmy, kama alivyojulikana zaidi, alifunga jumla ya mabao 357, huku mara mbili amewahi kupachika mabao matano katika mchezo mmoja.
Akiwa na miaka 20, alikuwa mchezaji mwenye umri mdogo kabisa kufunga mabao 100 katika Ligi ya England.
Wengi walifikisha idadi hiyo, wakiwa na miaka 25 au zaidi.
Ni mchezaji ambaye kila alipohamia klabu mpya, alifunga bao katika mchezo wake wa kwanza.
Alianza kuchezea klabu kubwa akiwa na miaka 17 alipojiunga na Chelsea na kufunga bao katika machezo wake wa kwanza 1957.
Alikuwa mfungaji bora wa ligi 1959 na 1961 na mabao yake 41 msimu wa 1960-61 hadi leo, ni idadi kubwa ya magoli kufungwa na mchezaji mmoja katika historia ya Chelsea.
Baada ya kuifungia Chelsea mabao 124, katika michezo 157 ya ligi katika kipindi cha miaka minne, Greaves alikwenda Italia kuichezea AC Milan na katika kipindi cha miezi michache aliokuwa nao, alifunga mabao 9 katika michezo 10.
Alirejea England na kujiunga na Tottenham Hotspurs kwa kitita cha pauni 99,000.
Kocha Bill Nicholson alisema, pauni moja ilipunguzwa ili fedha zisifikie laki moja kwa kuhofia kumpa kichwa kikubwa Jimmy na kujiona ni yeye tu England.
Aliichezea Spurs kutoka 1961 hadi 1970 na kuifungia mabao 266.
Baada ya hapo alijiunga na West Ham aliyoitikisia nyavu mara 13 katika mechi 38 msimu wa 1970-71.
Akiwa na Spurs, aliiwezesha kubeba Kombe la FA 1962 na 1967, Kombe la Washindi la Ulaya kwa kufunga mabao mawili katika ushindi wa 5-1 walipopambana na Atletico Madrid ya Hispania katika fainali 1963 na kuwa klabu ya kwanza ya England kuchukua ubingwa wa Ulaya.
Jimmy alikuwa mcheshi na mwingi wa masihara, baadhi ya wakati yaliyojaa maudhi. Lakini kama lipo tukio lilomuudhi ni siku ya fainali ya Kombe la Dunia katika Uwanja wa Wembley, wakati England ilipocheza na Ujerumani mwaka 1966.
Aliamini kuwa, alistahili kuwemo katika kikosi cha Sir Alf Ramsey baada ya kupona maumivu aliyoyapata katika michezo ya awali.
Badala yake, mtu aliyechukua nafasi yake, Geoff Hurst, alipewa nafasi kuendelea kucheza na yeye kuwa ubaoni.
Hurst alithibitisha uamuzi wa kocha ulikuwa sahihi kwa kufunga mabao matatu katika ushindi wa 4-2 katika mchezo uliokwenda muda wa ziada na England kubeba kombe.
Picha moja iliyopigwa siku ile ilionyesha wachezaji wa akiba wa England kwenye ubao wakisimama kushangilia ushindi.
Lakini Jimmy Greeves, alitulia tuli, kama vile mwenye masikitiko au aliyepigwa na mshangao.
Hata hivyo, Jimmy amekuwa akisisitiza hakuwa na kinyongo kuwekwa benchi, isipokuwa alikuwa haamini timu yao imebeba kombe kwa mara ya kwanza na pekee hadi hii leo.
Lakini kauli yake haipewi uzito kwa vile siku chache baadaye timu ilifanyiwa karamu ya ushindi, lakini Jimmy alisafiri na mkewe kwenda nje ya nchi kwa mapumziko, kitendo ambacho hakikutarajiwa.
Greaves ambaye alizaliwa East Ham, London, Februari 20, 1940 aliichezea timu ya taifa ya England kwa mara ya kwanza mwaka 1959.
Mshambuliaji huyu hatari wa hukumbukwa zinapozungumzwa fainali za Kombe la Dunia za 1962 zilizofanyika Chile.
England ilipocheza na Brazil, mbwa koko aliingia uwanjani, na wachezaji wote, pamoja na makipa, walishindwa kumkamata.
Lakini Jimmy, aliyekuwa pembeni akicheka pale wachezaji wenzake walipokuwa wanamfukuza mbwa huyo, aliamua kuingia katika msako.
Alimrukia mithili ya paka anavyomfanyia panya na yule mbwa alipokuwa akijaribu kujipapatua alimkojolea na ilimbidi aende kuvaa jezi nyengine na kurudi uwanjani.
Mshambuliaji hatari wa Brazil, Garincha alisema ule msako wa mbwa ulimfurahisha zaidi kuliko ushindi wa 3-1 walioupata katika mchezo ule wa robo fainali na dhidi ya England.
Garincha ambaye kwa mara ya pili mfululizo kule Chile, alichaguliwa mchezaji bora wa mashindano, aliomba awekewe yule mbwa na alienda naye kwake Brazil pamoja na Kombe la Dunia walilofanikiwa kulibeba baada ya kuifunga Czechoslovakia 3-1 katika fainali.
Garincha alisema, taifa la Brazil lililishinda kombe na yeye alishinda kupata mbwa, zawadi kutoka kwa rafiki yake Jimmy. Alimpa yule mbwa jina la JG, yaani Jimmy Greaves.
Siku ya mazishi ya Garincha (jina lake hasa Manuel Fransisco dos Santos) Januari 20, 1983 Jimmy alibeba picha ya Garincha akiwa na mbwa aliyemfanyia vituko kule Chile ambayo Garincha alimtumia.
Aliiweka picha ile aliyopelekewa na marehemu juu ya kaburi na kutamka: “Kwaheri rafiki mpenzi.”
Garincha na Jimmy walielewana na mara nyingi walifuatana baa kunywa pombe walipokutana. Kama pombe ilivyomharibu Garincha, nayo pia ilimtibua Jimmy na hata kulazwa hospitali ya wagonjwa wa akili.
Hata hivyo, Jimmy baadaye aliweza kuiacha wakati Garincha iliendelea kumtesa na kuchangia kifo chake haraka.
Jimmy alistaafu rasmi kucheza soka ya kulipwa mwaka 1971. Hata hivyo, alirudi uwanjani miaka saba baadaye kuichezea Barnet FC katika ligi ndogo ya England ya Kusini.
Aidha, aliichezea klabu ya Woodford Town FC kabla kuacha kandanda moja kwa moja.
Katikati ya miaka ya 1970, Jimmy Greaves alikabiliwa na matatizo ya kulewa kupita kiasi na hali yake kiafya na kiakili kuwa mbaya, lakini hatimaye mwaka 1978 aliweza kuiacha baada ya kupata matibabu hospitali ya wagonjwa wa akili.
Siku aliyoacha pombe, Jimmy alikunywa sana na kusema ukimuaga rafiki, lazima ufanye hivyo kwa furaha na si kwa kununa.
Alipoacha pombe, alianza kutangaza soka mpaka 1985 pale kipindi chake cha michezo kilipofutwa 1992.
Aidha, alishiriki katika vipindi vingi vya michezo vya vituo vidogo vya televisheni nchini England.
Pia alikuwa akiandika habari za michezo katika gazeti la The Sun na kujibu barua za wasomaji katika gazeti la Shoot katika miaka ya 1980 na 1990.
Katika mwaka 2002 jina la Jimmy liingizwa katika ukumbi wa wachezaji maarufu wa kandanda wa England.
Alifunga ndoa mwaka 1958 na sasa anao wajukuu.
Jimmy Greaves ni mchezaji ambaye hasahauliki katika historia ya klabu na timu ya taifa ya England pamoja na Kombe la Dunia kwa ufungaji wake wa mabao na umahiri wake wa kumkaba mbwa.
Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post | TrackBack URI for this post
Comments
Got something to say?

