Je, kuna makundi ya sheria katika usimamizi wa mirathi?
March 27, 2008
JAPHET PAGALE wa S.L.P 63304, Dar es Salaam anauliza: “Nimekuwa nikisikia kuwa suala la Mirathi linaweza kusimamiwa na makundi tofauti ya sheria, hivi hayo makundi ni yepi na yanatumikaje?” Kwanza nikushukuru sana ndugu yetu Pagale kwa swali lako zuri.
Kama ulivyouliza, ni kweli kuna makundi tofauti ya sheria zinazotumika kusimamia suala zima la mirathi. Makundi haya ya sheria ni kama ifuatavyo; Sheria za Serikali, Sheria za Kimila, na kundi la mwisho ni sheria za kidini (Dini ya Kiislamu). Kutumika au kutotumika kwa kundi fulani la sheria, kunategemeana sana na aina ya maisha ya marehemu aliyoishi hapa duniani, ama kama aliandika wosia, kama alitanabaisha kinagaubaga katika wosia huo kuhusu sheria gani itumike kusimamia mali zake pindi afapo.
Kwa ujumla iwapo mtu/marehemu hakuacha wosia, basi aina ya maisha aliyoyaishi yatatumika kuchagua aina ya sheria ya kusimamia na kugawa mali yake kwa warithi.
Hii ina maana kuwa, ikiwa marehemu aliishi maisha ya kufuata mila kwa bidii zake zote, basi sheria za kimila alizozifuata zitatumika ipasavyo; na akiwa alikuwa muumini wa dhati wa Uislamu, basi sheria ya Kiislamu itatumika. La hakuwa Muislamu na aliacha kufuata mila, ama alikuwa Mkristo basi sheria ya Kiserikali itatumika.
Kwa vile Japhet ametuuliza sheria hizi zatumikaje, basi leo hii ngoja tutazame swala la mirathi kama linavyotanabaishwa katika sheria ya kuandikwa ambayo wengine wanapenda kuiita sheria ya serikali.
Sheria ya kuandikwa yaani ile ya serikali inayotumika hapa kwetu Tanzania ni ile iliyotumika nchini India katika miaka ya 1865 na ililetwa hapa kwetu na Waingereza wakati wa utawala wao kupitia sheria ya matumizi ya sheria za India iliyoitwa Indian Acts (application) Ordinance, Cap.2 Kwa bahati zote mbili bado tunaendelea kuitumia hadi sasa – sheria hii inaitwa the Indian Succession Act of 1865.
Ikumbukwe kuwa sheria hii inatumika kwa Wakristo tu walioachana kabisa na mila au utamaduni wa makabila yao. Kwa ujumla sheria hii pia hutumika sana pale mtu anapofariki pasi na kuacha wosia juu ya namna mali zake anataka zigawanywe.
Kifungu cha 24 cha sheria hii kinasema kuwa mtu atahesabiwa kuwa amekufa pasi na kuacha wosia katika mazingira yafuatayo; Ikiwa hakuacha wosia kabisa; na ikiwa aliacha wosia ambao una upungufu na hivyo kuwa batili.
Kwa mujibu wa kifungu cha 26, mtu anapofariki pasi na kuacha wosia, basi mali yake itaangukia mikononi mwa mkewe au mumewe au watoto na ndugu wa karibu kabisa na marehemu. Sheria ya mirathi ya India imendelea kuchanganua masuala ya mirathi kama ifuatavyo;
Kifungu cha 27 kinasema kama marehemu ameacha mjane pamoja na watoto, basi theluthi moja (1/3) itaangukia mikononi mwa mjane. Sehemu iliyobakia itaangukia mikononi mwa watoto. Ikiwa hakuacha watoto basi nusu ya mali itakuwa ni ya mjane na nusu nyingine itaenda kwa ndugu wa karibu na marehemu. Ikiwa hakuna ndugu wa karibu wala watoto basi mali yote itachukuliwa na mjane.
Kifungu cha 28 kinasema kuwa kama marehemu hakuacha mjane basi mali yote itagawanywa kwa watoto au kwa ndugu wa karibu kabisa na marehemu. Ikiwa hakuna ndugu wala yeyote anayestahili kurithi katika ndugu basi mali hiyo itaangukia mikononi mwa serikali, yaani Kabidhi Wasii.
Vifungu vya 29 na 30 vinasema kuwa, baada ya kuitenga sehemu ya mjane (kama marehemu ameacha mjane) mali itagawanywa kwa watoto kwanza. Kama ni mtoto mmoja basi hiyo sehemu ya mali ukiacha sehemu ya mjane itaangukia yote mikononi mwa mtoto huyo. Kama ameacha watoto wengi basi itagawanywa kwa watoto wote kwa usawa bila kujali jinsia zao.
Ugawaji wa mirathi kwa warithi wengine (ikiwa marehemu hakuacha watoto) unatawaliwa na kanuni hi ya usawa kwamba hata kama itagawanywa kwa wajukuu lazima igawanywe kwa usawa pasi na ubaguzi wa kijinsia au kwa kufuata umri.
Kwa mujibu wa sheria hii, ndugu wengine kwa maana ya baba, mama, kina kaka na kina dada wanaweza kurithi mali ya marehemu kama hakuacha watoto. Ikitokea kuwa hakuacha watoto bali mjane, basi mjane atachukua nusu ya mali na ndugu watagawana nusu iliyobakia.
Sheria hii inawaruhusu pia warithi wa kike kurithi mali za aina yoyote ile, yaani mali isiyohamishika na ile inayohamishika tofauti na sheria za kimila ambazo zinawazuia warithi wa kike kurithi mali zisizohamishika.
Ikumbukwe kuwa sheria hii inamruhusu hata mume aliyefiwa na mkewe kurithi mali iliyoachwa na mkewe. Kwa mfano kama mke wakati wa kufariki aliacha nyumba ambazo alizichuma kwa jasho lake basi mume atakuwa na haki ya kurithi mali hizo. Lakini anayetazamwa kwanza ni mtoto.
Sheria pia imemtaja mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa kuwa hastahili kurithi mali ya marehemu baba yake bali mali ya mama yake isipokuwa kama amehalalishwa. Kwa maneno mengine kama wakati wa kufa kwa baba yake alikuwa hajahalalishwa, basi hatapata kitu, na kama akibahatika kuhalalishwa wakati wa uhai wa baba yake basi atastahili kurithi kama watoto wengine.
Kwa ujumla wake, sheria hii imejaribu kuangalia maslahi ya watoto pamoja na wale waliokuwa wakimtegemea marehemu ili wasiathirike kutokana na kifo cha mlezi au baba/mama yao.
Hii ndiyo sheria ya kiserikali inavyosema kuhusu suala la mirathi. Natumaini wakati tukiendelea kusubiri marekebisho yafanywe kuhusu sheria za mirathi, utakuwa katika nafasi nzuri ya kuamua kuishi maisha gani ili sheria ipi itumike pindi ufapo.
Lakini ninachoweza kushauri ni kujitahidi kuandaa wosia ambao ndiyo suluhisho kubwa katika mambo ya mirathi.
Kwa maswali, ushauri au maoni tuma kwa, magondza@yahoo.com, S.L.P 2616, Dar es Salaam, simu 07542-97051
Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post | TrackBack URI for this post
Comments
2 Responses to “Je, kuna makundi ya sheria katika usimamizi wa mirathi?”
Got something to say?


mume wangu alifariki, na msimamizi ni shemeji yangu. Sasa haki zangu nitazipata kweli? na mali baba mkwe ndio kazishikilia sasa hapo nitazipataje? Naomba ushauri.
Mimi baba yangu alikuwa mkisto alioa mke wa kwanza katika ndoa ya kikiristo lkn baadaye alioa wake wingi akiwemo mama yangu ambaye alizaa naye watoto tisa mama yangu alikuwa mke wa pili kuolewa baadaye baba alizaa na wanawake tofauti tofauti na baadaye kuoa mke wa mwisho ambaye aliishi naye mpaka kufariki kwakwe akazaa naye watoto wanne wawili wakiume na wawili wakike nakuwa na jumla ya watoto 28 alio watambua katika wasia wake
MMASWALI:
1)MJANE HALALI KISHERIA NI NANI?
2)WATOTO ALALI NI WAPI?
3)BABA ALIANDIKA WASIA AMBAO ULIWAPENDELI SANA WATOTO WA MKE WA MWISHO NA WATOTO WAKE WANNE WATOTO WAWILI TU WAKIUME WAMECHUKUWA KARIBU 48% YA MALI YOTE YA BABA HUKU WATOTO WENGINE 26 WAKIBAKIWA NA 52% NA MAMA YETU MWENYE WATOTO TISA HAKUPATA CHOCHOTE JE wasia waweza kuwa batili na kama ndio utaratibu gani kufuata kubatilisha kisheria? Asante kwa ushirikiano