Huu ni wosia wangu kwako Suleiman Nyambui
April 7, 2008
SALAAM aleikum wapenzi wasomaji wa safu hii ya Uwanja wa Kuchonga. Amani ya Bwana iwe nanyi.
Kama mtakumbuka wiki iliyopita Mzee wa Kuchonga alilia na ufisadi ambao hivi sasa umeshika kasi hapa nchini karibu katika kila sekta.
Mzee wa kuchonga aliweka hadharani machozi ya wadau wa riadha jinsi walivyoathirika kwa usanii na ufisadi uliofanywa na baadhi ya viongozi wa Chama cha Riadha Tanzania (RT).
Unaweza kusema ni jambo dogo, lakini katika fani ni ufisadi wa hali ya juu, ambao unaweza kuufananisha na sakata la Richmond na mengineyo ambayo yanaliyumbisha taifa la Tanzania kiuchumi hivi sasa.
Wahenga husema mwenye macho haambiwi ona, pia mkubwa hakosei na akikosea huwa bahati mbaya.
Tunapenda kuamini hivyo, na ndivyo ilivyotokea kwa Chama cha Riadha Tanzania (RT), baada ya Chama hicho kufanya yale ambayo hayakutarajiwa na watu ambao hawakutarajiwa kutokana na hadhi, historia na umri wa wahusika.
Tanzania wiki iliyopita ilishindwa kushiriki mashindano makubwa ya mbio za nyika ya dunia, huko Scotland ambako kati ya mambo yaliyochangia ni kitendo cha Katibu Mkuu wa RT, mwanariadha mkongwe na mwenye historia kimataifa, Mujaya Suleiman Nyambui, ambaye aliwasilisha orodha ya majina ya msafara wa timu hiyo ambayo mengine yalizua utata katika Ubalozi wa Uingereza.
Kutokana na utata huo, utaratibu mzima wa timu hiyo kupewa viza, na hata baada ya uhakiki na ukweli ulipopatikana tayari muda ulikuwa umepita na hivyo Tanzania kupoteza nafasi hiyo.
Kukosekana kwa Tanzania kushiriki mashindano hayo kumeathiri mambo mengi na kulitia aibu taifa, kwani kitu kilichosababisha hali hiyo, kilifanywa na watu ambao umma wa Watanzania, hususan wadau wa riadha wamewapa majukumu hayo.
Hakika, utashangaa na huwezi kuamini, lakini ndivyo watu wenye hadhi na heshima zao waliokabidhiwa majukumu hayo, walilikifanya na kulitia aibu taifa.
Ni aibu, na ili hali ya hewa irudi katika hali yake, uwajibikaji lazima uwepo.
Hakuna kuoneana huruma, wala izan, ila ukweli ndio huo.
Sikiliza kilichofanywa na RT, hususan mtendaji wake mkuu Nyambui, ambacho kimeandika historia katika medani ya michezo.
Ukweli ni kwamba haliepukiki, lakini limetokea na baya zaidi limeandika historia mbovu na mbaya katika sekta ya michezo hapa nchini.
Bila shaka Watanzania watakuwa bado na kumbukumbu kutokana na kile kilichotokea wiki iliyopita na kupamba vyombo mbalimbali vya habari.
Hivi sasa nchi imetoka kwenye kashfa kadhaa za ufisadi, zilizotokana na mikataba mibovu ya Richmond, fedha za EPA na nyinginezo, ambazo madhara yake katika uchumi wa Mtanzania hivi sasa anayapata yule wa ngazi ya chini. Mvuja jasho.
Hebu sikia mambo ya Nyambui na wenzake. Eti katika kukisaidia chama hicho cha riadha, Katibu huyo Mtendaji alijitosa kusaka wadhamini na baada ya kuwapata, akawaahidi fadhila ya kuwasaidia kupata viza ili nao waende nchini Scotland ama kutalii, kufanya ‘shopingi’, au shughuli zao wenyewe, binafsi.
Inashangaza RT kuacha kushughulikia masuala ya riadha na kuibuka wafanyabiashara wa viza.
Aibu hii ambayo inazidi kuipaka matope Tanzania katika medani ya michezo kimataifa, imeletwa na RT au AT.
Kukosa uaminifu na vitendo vya ufisadi vilivyofanywa na Nyambui na wenzake, ndivyo vilivyoiaibisha sekta ya michezo safari hii.
Tunashangaa hadi leo, serikali kushindwa kulitolea taarifa suala hili licha ya wahusika kukiri kuitwa hadi Ikulu, ambako wanatamba walieleza yaliyotokea na mambo yameisha.
Sijui kama ni kweli, tunasubiri, yetu macho na masikio.
Timu hiyo, kwa mujibu wa Nyambui, ilikuwa inaundwa na wachezaji 19 na viongozi 12 na taratibu za kuwaombea viza tayari kwa safari hiyo zikaanza.
Hapo ndipo mambo yakaibuka katika Ubalozi wa Uingereza jijini Dar es Salaam, katika ufanyaji kazi wake, ikajulikana kuwa kuna udanganyifu mkubwa umefanywa na RT, hasa kwenye idadi ya viongozi na wachezaji.
Ubalozi huo ukafanya unachokijua kwa usalama wa nchi yao, ambako ikabainika kuwa kuna upungufu, au udanganyifu kwani baadhi ya watu waliorodheshwa maelezo yao yalikuwa na utata.
Ukaamua kukataa kugonga viza hizo na ukafanya utafiti wake, ikiwamo kuwasiliana na mmoja wa wajumbe wa chama hicho, ambaye pia ni mdau mkubwa wa riadha hapa nchini, Filbert Bayi na ikabainika kuna walakini.
RT ikajulishwa juu ya hilo, lakini iliendelea kuwang’ang’ania ‘watalii’ hao, hasa kutokana na walichokuwa wamekipata Nyambui na wenzake.
Ukweli zaidi unabainisha kuwa, safari hiyo iligeuzwa mradi na viongozi hao wa RT na tena inahisiwa una harufu ya rushwa na ufisadi, hasa kutokana na jambo hilo kuendeshwa kisiri tofauti na safari nyingine zinazozihusu timu za taifa za riadha.
Katika msururu huo, RT iliyowaingiza watu hao inadai walikuwa ni wafadhili ambao walisaidia kufanikisha safari hiyo, kifupi unaweza kusema ilikuwa inalipata fadhila.
Nyambui, msomi na mtu mwenye historia katika medani ya riadha, akaamua kuingiza hao anaodai wafadhili wake na wengine marafiki au ndugu.
Kinachotia shaka si kuwajumuisha watu hao katika safari hiyo, lakini ni usiri uliokuwepo katika kulifanya hilo.
Wafadhili hao wakiwamo viongozi wa Chama cha Riadha Zanzibar (ZAAA), hatimaye waliingizwa katika msafara huo.
Biashara hiyo haramu ambayo imebainika kuwa ilikuwa ni mchezo wa muda wa chama hicho, safari hii imelitia doa taifa na wahusika wanajuta.
Mchezo huo mchafu, ndio ulioitia hasara Tanzania hususan wachezaji, kwani kwa kushindwa kushiriki mashindano hayo makubwa, nchi imekosa mengi na kuwapunguzia uzalendo wachezaji.
Haina ubishi, Tanzania imepata pigo kwa sababu ya watu wachache, ambao wamekiri walichokifanya.
Nyambui amekiri kuwa wafadhili hao aliwatambulisha kama viongozi, huku wengine akiwaweka kundi la wachezaji, akiwamo mtoto wa Katibu wake Msaidizi, Julius Murunya Musomi. Je, huo ndio utaratibu na usajili wa vyama vya michezo ikiwamo RT, ndivyo unavyoelekeza?
Kwa ufisadi huu, hata Nyambui uombe msamaha vipi, umekiri, ni kashfa ambayo haiepukiki kwako hata kwa Musomi, hivyo kuwajibika ni lazima.
Ukimya wa serikali utatufanya tuzue au tujadili mengi, kuna nini hapo? RT wamekiri kuonyana na kupeana karipio, si hoja, na haina mshiko.
Kwa haya yote, Nyambui umekiri kuyafanya, imani yako na ya chama imeshuka kwa kiwango kikubwa, kwani mmelitia aibu taifa na sekta ya michezo.
Muwajibike, na huu ndio wosia wa Uwanja wa Kuchonga kwako, Mujaya Suleiman Nyambui. Wajibika, usisubiri nguvu ya umma.
‘Aluta Continua’, tukutane wiki ijayo.
Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post | TrackBack URI for this post
Comments
Got something to say?

