Hongera Standard Chartered, Barrick

October 29, 2007

MWISHONI mwa wiki yalifanyika matukio mawili katika medani ya michezo hapa nchini. Moja ni kumalizika kwa mashindano ya Kombe la Taifa ya mpira wa kikapu na na jingine ni la Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Muhammed Seif Khatib, kuzindua mashindano ya kimataifa ya mbio za marathoni ya Standard Chartered.

Mashindano hayo ya kikapu, ambayo kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), hufanyika kila mwaka. Lakini kwa miaka kadhaa yamekuwa yakisusua na wakati mwingine kutofanyika kabisa kutokana na ukata unaovikabili vyama ama mashirikisho mbalimbali ya michezo.

Mashindano hayo yaliyomalizika mwishoni mwa wiki, yamefanyika baada ya kupigwa kalenda kwa takriban mara tatu, kutokana na TBF kutokuwa na fedha za kuyaendesha.

Jahazi hilo liliokolewa baada ya Kampuni ya uchimbaji madini ya Barrick, kujitosa kuyadhamini kwa sh milioni 50, huku Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) nayo ikichangia sh milioni 15 na hivyo kufanikisha kufanyika kwa mashindano hayo ambayo yalishirikisha mikoa 11 ya Tanzania Bara na Visiwani.

Wakati mashindano hayo ya kikapu yakimalizika, Waziri Khatib alizindua mbio hizo, ambapo pia benki hiyo imeidhamini timu ya Tanzania ya wanaume na wanawake.

Waziri Khatib aliipongeza benki hiyo, kwa kuidhamini kwa mara pili timu hiyo ya wanariadha ya Tanzania, kwani hata mwaka jana ilifanya hivyo.

Waziri huyo alizidi kuipongeza benki hiyo, si kwa kuamua kufadhili tena mwaka huu, bali pia mwaka huu, wameongeza ufadhili kwa wanawake.

Wanamichezo hao wa mpira wa kikapu na riadha kupata nafasi ya kushiriki mashindano hayo si faida kwao pekee, bali pia kwa maendeleo ya jumla ya michezo hapa nchini.

Timu hizo kushiriki mashindano mbalimbali ni moja ya nafasi za kuinua viwango vyao, kupata uzoefu na kulitangaza taifa kimataifa.

Kutokana na hali ya ukata na uhaba wa wadhamini katika shughuli mbalimbali za michezo hasa nje ya soka, ambao umekuwa ukikimbiliwa na wafadhili wengi, ni kitendo cha kuungwa mkono.

Michezo mingi hususan riadha na kikapu, kwa miaka mingi imekuwa taabani kifedha, huku pia wafadhili au wahisani wakiwa ni wachache au kutokuwepo kabisa katika michezo hiyo.

Tumekuwa tukishuhudia, timu nyingi aidha za klabu au timu za taifa zikishindwa kwenda kushiriki mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi, na tatizo ni ukata.

Vitendo vya makampuni, hayo kusaidia riadha na kikapu havina budi kuungwa mkono na wadau mbalimbali wa maendeleo ya jamii na kuacha ile kasumba ya kuegemea zaidi kwenye soka.

Pia, vyama husika vinatakiwa kujipanga, kujenga mahusiano mema na asasi mbalimbali sambamba na uwazi katika kuitumia misaada hiyo wanayopewa au kufadhiliwa ili kulinda uhusiano mzuri, kwa maendeleo ya michezo husika.

Kwa upande wa wachezaji nao hawana budi, kulipa fadhila hizo kwa kujituma na kufanya vema katika mashindano mbalimbali.

Tunapenda kuwapongeza Standard Chartered na Barrick kwa kuikumbuka michezo hiyo na wasiishie hapo bali, wawakumbuke na vijana wadogo ambao ndio tegemeo la kesho na chimbuko la vipaji katika michezo mbalimbali.

Tunasema hongera Standard Chartered na Barrick na msiishie hapo