Hongera Japheth Kaseba
November 26, 2007
JUZI usiku, Tanzania iliingia katika rekodi ya aina yake baada ya Japheth Kaseba kutwaa ubingwa wa dunia wa mchezo wa kick boxing kwa kumshinda, Abhijeet Pektar wa India, aliyekuwa akishikilia taji hilo.
Pektar, aliyekuja nchini akiwa bingwa mtetezi wa dunia uzito wa kilo 79 na bingwa wa bara la Asia, kwa umahiri wa Kaseba, bondia huyo, anaondoka nchini akiwa si bingwa wa dunia.
Hii ni baada ya Kaseba kufanya kweli katika pambano hilo lililofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam kwa kushinda kwa KO katika raundi ya kwanza.
Pambano hilo lililovuta hisia za wengi waliokuwa na shauku ya kuona nini anafanya Kaseba katika pambano hilo, waliishia kushangilia baada ya shujaa huyo wa Tanzania kutangazwa mshindi.
Tukiwa sehemu ya wadau, hatuna budi kumpongeza Kaseba binafsi kwa kuiletea nchi heshima kubwa kwa sababu, kujituma kwake na kuzingatia mafunzo ya kocha wake, ni kati ya sababu zilizomwezesha akashinda.
Huu ni ushindi mkubwa si kwa Kaseba pekee, bali kwa sekta ya michezo na Tanzania kwa ujumla, kwa sababu, Kaseba alikuwa akipigana ulingoni kwa jina la Tanzania.
Kwetu wa Tanzania Daima, tunampongeza Kaseba kwa mafanikio makubwa yaliyoipa Tanzania sifa kubwa nje ya mipaka.
Aidha, ushindi huu pia unaleta changamoto kubwa kwamba, kuna michezo mingi ambayo kama itapewa umuhimu mkubwa, yaweza kuiletea sifa na heshima kubwa Tanzania.
Hivyo, ni wito wetu kwa serikali, kampuni, mashirika na taasisi kadhaa, ziwe za serikali au binafsi, kugeukia michezo mingine badala ya kuelekeza nguvu katika soka pekee.
Tunasema hivi kutokana na mazingira halisi kuwa, michezo kwa sasa si burudani tena, bali ni ajira, hivyo kama msukumo utaelekezwa kwa michezo yote, sekta ya michezo itakuwa na tija kubwa.
Ingawa soka ndiyo yenye wapenzi na mashabiki wengi, lakini Tanzania ina vijana wenye vipaji mbalimbali, ambao kama watapata sapoti, vipaji hivyo vitakuwa vya manufaa kwao na taifa.
Ni wito wetu kuwa, msukumo usiwe katika soka pekee bali kwa michezo yote, kwa sababu si vijana wote wenye kipaji cha soka.
Kwa mantiki hiyo, sekta ya michezo kwa ujumla iwe ya manufaa kwa vijana wetu na taifa, michezo yote ipewe uzito unaostahili bila kujali wingi wa wapenzi na mashabiki.
Aidha, hatuna budi kuwapongeza pia wote walioshiriki kwa namna yoyote ile, ikiwamo kumwandaa Kaseba na maandalizi ya pambano kwa ujumla, kwani siri ya mafanikio ni maandalizi bora.
Ushindi huu pia una ujumbe mzito ndani yake kwamba, kama sekta hii itaondokana na matizo mbalimbali yanayoisonga, ikiwamo migogoro, inaweza kupiga hatua kubwa.
Ni wito kwa viongozi wa klabu na vyama vya michezo mbalimbali pia, kutimiza wajibu wao kwa lengo la kuinua michezo nchini, tukiamini hili linaweza kufikiwa kwa kuwapo mipango bora, amani na mshikamano.
Hivyo, kwa vile ushindi huu wa Kaseba, ni fahari kubwa kwa mchezo wa kickboxing, sekta ya michezo na Tanzania kwa ujumla, pia uwe changamoto kwa vyama kujipanga vema.
Kwamba, kama vitakuwa na mipango mizuri pamoja na utekelezaji, huku ukiwepo ushirikiano mzuri baina ya vyama, wadau na serikali, hakuna kitakachokwamisha mandeleo ya michezo nchini.
Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima

