Hatuwezi kuendesha nchi kwa fitna
August 20, 2008
NINAENDELEA na mada niliyoianza wiki iliyopita ambayo niliahidi kuendelea nayo leo kutokana na ukweli kwamba masuala niliyojadili yalihitaji muda mrefu zaidi kuyajadili na pengine kuyachanganua.
Ni jambo jema kwamba umuhimu na haja ya kuendelea na mada hizo ambazo naweza nikakiri mapema kwamba nilizifanyia tafakuri kwa sehemu zimeendelea kugusa hisia za watu mbalimbali hata baada ya makala yangu kuchapishwa Jumatano ya wiki iliyopita.
Mada ya kwanza katika hizo ni ile inayohusu hadhi ya Zanzibar katika muungano ambayo leo hii inatajwa kuwa ajenda kubwa ya kitaifa inayouweka utaifa wa Tanzania katika nafasi ngumu kabisa ikiwa ni miaka zaidi ya 44 tangu nchi mbili jirani zilipoungana na kuunda nchi, dola na pengine taifa moja.
Siku moja baada ya kuhoji kupitia safu hii kuhusu kukosekana kwa misingi imara ya uwajibikaji wa pamoja baina ya serikali mbili za Chama Cha Mapinduzi (CCM), ile ya muungano kwa upande mmoja na ya Zanzibar kwa upande mwingine, kulikojidhihirisha katika siku za hivi karibuni, Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, aliweka mguu wake katika mada hiyo na akajikuta akiwasha upya hasira na pengine uzalendo wa Wazanzibari katika kupigania hadhi ya visiwa vyao viwili.
Hali ya kukosekana kwa uwajibikaji wa pamoja inayokwenda sambamba na kuporomoka kwa nidhamu ya kazi, heshima na utii miongoni mwa viongozi wa kiserikali na wale wa ndani ya CCM inaelezwa na baadhi ya wadadisi wa mambo kuwa hatua moja inayoweza kusababisha taifa hili kusambaratika na kurejea kule tulikotoka, zilizokuwa nchi za Tanganyika na Zanzibar.
Kwa hakika kabisa, mimi pia nalazimika kuungana na wenzangu wenye fikra hizo hata kudiriki kusema pasipo hofu kwamba, hali hii ya mambo ni ushahidi kwamba, baadhi ya viongozi wa juu wa serikali zote mbili na wa chama hiki tawala wamefikia hatua ya kutaka kutupeleka wanakotaka twende tena kwa masilahi yao wenyewe.
Dalili za CCM na serikali zake zote mbili kuporomoka na hata kuelekea kupoteza uhalali wa kuliongoza taifa kwa mantiki ya visheni, umoja, mshikamano na uwajibikaji wa pamoja zilianza kuonekana miaka ya mwanzo ya 1990 enzi Ali Hassan Mwinyi akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na John Samwel Malecela akiwa Waziri Mkuu wake, na baadaye hali hiyo ikaendelea hata alipokuja David Cleopa Msuya, kuwa Waziri Mkuu.
Ushahidi wa mambo haya uko wazi kabisa kwani ni katika kipindi hicho kulizuka suala la Zanzibar kutaka kuingia katika Jumuiya ya Kiislamu Duniani (OIC) na pia kukaibuka hoja ya kundi la wabunge 55 maarufu kama G 55 waliotaka kuundwa kwa serikali tatu katika muungano wakiililia Tanganyika yao.
Ufa mkubwa wa kiuongozi na kuporomoka kwa kasi kwa uwajibikaji katika kipindi hicho, ulifanikiwa kuzalisha shujaa mmoja, Augustine Mrema wakati huo akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani na baadaye kidogo akavishwa joho la kuwa Naibu Waziri Mkuu akifanya kazi chini ya Malecela.
Ghafla, hali hii ikamfanya Mrema aibuke na kuwa kipenzi nambari moja cha wananchi walalahoi na akautumia vema udhaifu na kupoteza mwelekeo kwa serikali kujiimarisha kisiasa akiongoza mapambano ya kukabiliana na majambazi, majangili, wabadhirifu wa mali na rasilimali za taifa na pia mtetezi wa haki za wanawake ambao wakati huo walionekana kudhulumiwa sana.
Hali hii ya mambo kwa kiwango kikubwa ikitumika kuuficha udhaifu wa kiuongozi na kioganaizesheni wa Rais Mwinyi na serikali yake nzima na silaha pekee aliyobakia nayo rais wakati huo ikawa ni uadilifu wake binafsi, hulka yake ya kutopenda makuu na dhamira yake ya wazi ya kuruhusu na kuyapokea kwa mikono miwili mabadiliko yote makubwa yawe ni ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Leo, udhaifu ambao tuliuona zama za Mwinyi na ukafichwa kwa kiwango kikubwa wakati wa kipindi cha miaka mitano ya mwanzo ya utawala wa Benjamin Mkapa (1995-2000) kabla ya hali kubadilika baadaye, unaonekana kutaka kurejea tena hapa nchini kwa namna na njia ambayo kimantiki haitofautiani sana na ilivyokuwa wakati wa Mwinyi.
Matokeo yake yako bayana. Hali ya mambo inaonyesha wazi kwamba, taifa limeanza kupita katika kipindi cha kupwaya na kukoma kwa utawala wa kisheria na watu kuchukua madaraka kinyemela wakiwa na uwezo wa kufanya, kutenda na kusema lolote, liwe la heri au la shari.
Ushahidi wa hali hii uko dhahiri, leo hii katika utawala wa Rais Kikwete, mtu yeyote, tena kiongozi, awe waziri, mkuu wa mkoa, mbunge, spika, mwanasheria mkuu, anao uwezo wa kusimama akitumia mamlaka aliyonayo na akampa jina baya au zuri yeyote atakaye kwa sababu tu ya kulinda masilahi yake binafsi au ya kundi analolitumikia na kuliabudu kama si kuliamini.
Nimepata kuliandika hili na leo narejea tena kuligusia. Ndani ya serikali ya Kikwete leo, kuna mawaziri na naibu mawaziri wanaojipambanua waziwazi kwamba wao ni marafiki au maadui wa wazi wakikubaliana ama kupingana si kwa hoja za msingi bali kwa sababu ya hulka zao za kugombea tamu ya madaraka na wakati mwingine malengo yao ya kisiasa ama ya mwaka 2005 au ya huko tuendako mwaka 2010 na wakati mwingine mwaka 2015.
Hali hiyo ya mambo imefikia hatua ya kuitikisa nchi kwa kiwango cha kukatisha tamaa hata kusababisha sumu yake ikapenyezwa kuanzia serikalini, ndani ya Bunge, Baraza la Wawakilishi na hata katika ngazi ya CCM taifa.
Matokeo ya uteketeke huu wa mambo unawafanya viongozi wa juu wa CCM na wale waliopo serikalini waishi kwa kujikagua mara mbili mbili, wakikaa kwa staili ya kuviziana, kulipuana, kuzushiana vifo, uchawi, ufisadi na kila aina ya uchafu ambao kimsingi umeota mizizi ndani ya chama hicho tawala na pengine serikalini kwa miaka mingi sasa.
Hali hii ya viongozi wa juu wa serikali na CCM ‘kushikana uchawi’ na kunyosheana vidole imesababisha viongozi serikalini, bungeni na hata katika ngazi ya taifa ya chama hicho tawala wajikute wakigawanyika katika makundi ya kisiasa yaliyoota na kushamiri kwa nguvu ambayo haijapata kuwapo kabla.
Kwa sababu hiyo basi ndiyo maana ukiangalia kazi za wazi na zisizo za wazi ambazo leo hii zinafanywa na wasaidizi wa Rais Kikwete kwa mfano kama walivyo kina January Makamba, Salvatory Rweyemamu, Premmy Kibanga na wengine wengi, unaweza ukapigwa butwaa ukishangaa iwapo watu hao ni wanasiasa, wapambe, watendaji wakuu serikalini au wasaidizi wa rais kwa maana halisi ya wajibu wao.
Katika misingi hiyo hiyo ni jambo la kusikitisha kwamba, leo ile falsafa ambayo ndiyo imekuwa ikitumika katika medani ya soka hata kupewa jina la ‘fitna za soka’ inayojumuisha majungu, uzushi, kuzungukana, usaliti, kutishana, ubabe na mambo yanayofanana na hayo ndiyo inayotaka kutumika kuendesha serikali, Bunge, vyama vya kisiasa na vyumba vya habari.
Leo, zile nguzo kuu tatu za dola (zilizo rasmi na zisizo rasmi), Serikali, Bunge na Vyombo vya Habari, zimegeuka kutoka kuwa taasisi za msingi katika kuonyesha njia sahihi ya kimaendeleo na kuwa majukwaa ya porojo za kisiasa zenye malengo ya kushikana uchawi, kuzushiana, kupindisha mambo na kutishana.
Katika gonjwa hili jipya, mahakama ambazo kwa miaka mingi zimekuwa zikishutumiwa kwa rushwa ndizo zinazoweza kusimama kama taasisi huru inayofanya kazi kwa kuzingatia maadili mema ya kikazi.
Watu wote makini ambao wamekuwa wakifuatilia masuala nyeti na yanayogusa hisia za Watanzania kama Richmond, EPA, mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar, mjadala wa Zanzibar ni nchi au la na tukio la hivi karibuni kabisa la kifo cha Chacha Wangwe, wanaweza wakawa mashahidi wa namna ya kuzushiana, kuhukumiana, kukejeliana, kutukanana, kudhalililishana, kunyanyasana na matendo mengine yanayofanana na hayo, kunavyotumika kupotosha na kuharibu hali ya hewa kisiasa na kitaifa.
Ni jambo la bahati mbaya kwamba, kila unapojaribu kufuatilia kwa hatua suala moja baada ya jingine katika hayo niliyoyaorodhesha, ili kupata ukweli halisi wa kitu gani hasa kipo nyuma ya kila mojawapo ya hoja hizo, unakutana na ufisadi wa fedha, mawazo na matendo mengine yakiwamo yale yanayotisha.
Lakini pengine baya zaidi kuliko yote ni kwamba, mambo yote haya machafu yanayotokea leo hii tena yakiratibiwa na kuongozwa na baadhi ya viongozi tuliowapa dhamana kubwa ya kutuongoza na kututoa katika matatizo lukuki ya ufukara hata kuifanya nchi yetu ifanane na lile neno lililoandikwa katika moja ya vitabu vya kiimani likimzungumzia ‘kipofu kumuongoza kipofu mwenzake’.
Ni jambo la hatari na kuanza kuliogopa leo hii tunapowaona wale viongozi wanaoratibu ajenda za namna hii leo hii, kuwa ndiyo wale wale au watangulizi wao waliojaribu tuamini kwamba, mke wa mzee Mwinyi, Mama Sitti ndiye aliyekuwa akishika hatamu za kiuchumi za taifa hili zama mumewe akiwa madarakani. Leo tumethibitisha ulikuwa uongo.
Hawa ndio watu ambao walijenga hoja na wakasema mara nyingi hata tukaamini kuwa, Frederick Sumaye, ambaye hata kwenye orodha ya mafisadi iliyotolewa na Dk. Willibrod Slaa hakuwamo, zama akiwa Waziri Mkuu alikuwa miongoni mwa Watanzania matajiri wa kutupwa kwa sababu ya kujiwekea mamilioni ya fedha nje ya nchi na kukwapua kila alipoweza. Leo hatua kwa hatua uzushi huo umeanza kubatilika.
Hawa ndio watu waliosimama kidete na kutaka watuaminishe Watanzania kuwa Chama cha Wananchi (CUF) ni chama cha Wapemba na Waislamu, kilicho na malengo ya kuibadili nchi ili ianze kufuata sharia na kisha kufungua makao ya genge la Al Qaeda hapa nchini. Wengi wetu tulishagundua janja hii batili na sasa imebakia historia.
Ni watu hawa hawa ambao miaka ya 1990 wakiwatumia baadhi ya wanahabari ambao leo wamewapa malipo mema, walitumia vyombo vya habari kuwaaminisha Watanzania kuwa Mzee John Samwel Malecela, alisilimishwa kuwa Mwislamu kule Iran na akapewa jina la Kiislamu ili kumuandaa kuwa Rais wa Tanzania baada ya Mwinyi mwaka 1995. Hili nalo limepita na kuthibitisha uongo wa wazi wa wanasiasa wa kundi hili.
Ni watu hawa ambao walifikia hatua ya kuwaaminisha Watanzania kuwa, Profesa Mark Mwandosya ndiye kiongozi aliyeshiriki kikamilifu tena yeye binafsi kuliuza kwa bei ya kutupa na kitapeli lililokuwa Shirika la Posta Tanzania, ilihali wakijua kwamba uamuzi huo ulifikiwa na Baraza la Mawaziri kwa kauli moja na wao wenyewe wakiwamo serikalini.
Hawa ndio watu wale wale waliofanya juu chini kutuaminisha kuwa Dk. Salim Ahmed Salim ni Mwarabu asiye na mapenzi ya kweli na nchi yake na mtu aliyekuwa na uhusiano wa moja kwa moja na wapinzani wa mapinduzi ya mwaka 1964 ya Zanzibar, na kuwa alipanga kuwarejesha ndugu zake hao kuchukua madaraka visiwani iwapo angeshinda urais. Leo hii kila mwenye akili anajua matokeo ya uongo huo.
Ni jambo la fedheha kwamba wanasiasa wale wakiwatumia baadhi ya mawakala wao wale wale na wengine wapya waliowazalisha kwa nguvu ya shekeli walizonazo, wameanza tena kutengeneza uzushi mpya dhidi ya yeyote wanayemuona kuwa tishio dhidi yao kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Tunaambiwa ndani ya chama chao wanaolengwa wamefikia 71 wakiwamo kina Malecela, Samuel Sitta, Aloyce Kimaro, Harrison Mwakyembe na wengi wengine, huku baadhi ya maadui zao wengine wakiwa nje ya chama hicho, kwa kuwataja wachache; Dk. Slaa, Reginald Mengi, Freeman Mbowe, Zitto Kabwe na John Mnyika. Tuombe Mungu wasifanikiwe.
Tukutane wiki ijayo Mungu akipenda.

