Hali yazidi kuwa mbaya Kenya

January 29, 2008

MAPIGANO ya kikabila yanayoendelea nchini Kenya yanazidi kuifanya hali ya amani nchini humo ambapo katika muda wa siku tatu za mwishoni mwa wiki iliyopita zaidi ya watu 92 wameripotiwa kuuawa huku nyumba zaidi 800 zikiwa zimeteketezwa kwa moto.

Katika eneo la Naivasha nje kidogo ya Jiji la Nairobi, maiti zaidi ya 28 zilikuwa zimeokotwa na polisi huku maiti zaidi ya 64 zilikiwa zimehifadhiwa katika hospitali ya Nakuru baada ya kukutwa zimetupwa sehemu mbalimbali za mji huo ambao ulikumbwa na vurugu kubwa kuanzia mwisho wa wiki iliyopita.

Katika eneo la Nakuru jana siku nzima ulikuwa ni uwanja wa vita baina ya polisi na watu ambao walikuwa na silaha za jadi kuendeleza mauaji. Polisi walilazimika kurusha risasi za moto hewani pamoja na mabamu ya machozi ili kuwatawanya watu hao.

Katika eneo la Naivasha, polisi walitumia helkopta kulinda amani katika eneo hilo ambalo lenye zaidi ya wafanyakazi 20,000 wa mashamba ya maua.

Taarifa zaidi zimeelza kuwa nyumba 800 zimeteketezwa kwa moto katika eneo la Timboroa lililoko kwenye Jimbo la Rift Valley katika ghazia zilizoanza Ijumaa wiki iliyopita hadi jana mchana.

Kufuatia mauaji hayo, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan ambaye yuko nchini humo kwa ajili ya kutafuta suluhu ya mgogoro wa kisiasa nchini humo, alishauri kuwa wanajeshi wapelekwe kwenye maeneo yote yenye ghasia kutuliza na kulinda amani.

Pamoja na mauaji hayo, Rais mstaafu wa Kenya Daniel Arap Moi ameripotiwa kulazwa hospitali ya mjini Nairobi akikabiliwa na maumivu ya mgongo na Daktari wake alitaarifu anaendelea kupata matibau

huku mmoja wa viongozi wa ODM ambaye ni Mbunge wa Eldoret Kaskazini, William Ruto akiwataka wananchi kuacha mauaji yanayoendelea nchini humo.

Pia Rutto alikaririwa na gazeti la The Nation nchini Kenya akisema kuwa mauaji yanayoendelea hayawezi kuhusishwa na masuala ya ukabila bali yanatokana na maovu yaliyofanywa na watu wachache walioamua kuvuruga matokeo ya uchaguzi huo kwa makusudi.

“Ninawaomba watu wetu waache mapigano, tunajua kuwa wale waliopotosha matokeo ya uchaguzi ndiyo walionuia kutuweka katika hali hii, lakini ninawaomba pia tusishawishike kubadili siasa kwenye sura ya ukabila, siasa inahusiana zaidi na masuala ya sera, maendeleo na ilani, tunachotakiwa ni kujenga heshima na umoja,” alisema Ruto.

Viongozi wengine wa ODM, Raila Odinga na Musalia Mudavadi walivilaumu vyombo vya usalama nchini humo kwa kusimamia upande mmoja na kudai kuwa hatua hiyo ni kinyume cha sheria.

“Polisi hawatakiwi kuegemea upande mmoja, inakuwaje watu wanauawa, wananyang’anywa mali zao na wengine wanabakwa wakiwa njiani kuelekea maeneo ya magharibi mwa Kenya, huku Polisi wakidai kuwa wanafanya doria katika maeneo hayo?” alihoji Odinga.

Naye Mudavadi alisema kuwa chama chake kinafuatilia kwa makini hali ya kutokuwepo kwa amani, ” kuingizwa kwa jeshi mitaani si hatua nzuri, hizi ni dalili mbaya, hili ni suala la kubebwa na polisi na vyombo vingine vya usalama wa ndani, si jeshi.”

Pamoja na juhudi hizo, taarifa za jana mchana zilisema kuwa mauaji yaliyotokea Naivasha juzi yamesababisha mgomo wa kutwa nzima jana katika maeneo mengi ya Magharibi mwa Kenya, yakiwemo Kisumu, Kakamega, Kapsabet, Gilgil, Migori, Busia na Eldoret, baada ya taarifa kuwa uvamizi huo ulipangwa na jamii yao.

Mgomo huo ulioambatana na maandamano uliibuka baada ya Kamishna wa Polisi Hussein Ali kutangaza kuwa wanatarajia kuwafungulia mashtaka ya mauaji watu 28 kutokana na kudaiwa kushiriki katika machafuko yanayoendelea nchini humo, bila kutaja majina ya watu watakaoshtakiwa.

Wakati machafuko hayo yakiendelea mjini Naivasha na kufanya idadi ya vifo katika mji huo pekee kufikia 28, tayari pia mji wa Kakamega umeathirika kutokana na kuchomwa moto kwa nyumba na duka wakati wa mapambano ya Polisi na watu wenye sialaha jana asubuhi.

Vurugu hizo ziliendelea jana mchana katika miji ya Kisumu na Migori, makundi ya vijana yakiwasha moto na kuweka vizuizi barabarani huku wakiimba nyimbo za kukisifia chama cha ODM.

Huku wakiwa na mabango waliripotia kuingia katika baadhi ya shule na kuwafukuza wanafunzi wakidai kuwa “Bila Raila hakuna shule”, huku wakichoma mataidri na kuzuia watu kutoka au kuingia mjini humo kwa kutumia barabara za Kisumu-Nakuru na Nakuru-Busia.

Mamia ya wafanyakazi wa umma mjini Kisumu pia walilazimishwa kurejea makwao asubuhi kwa ajili ya usalama wao, baada ya vijana hao kusamba katika mitaa yote.

Katika miji ya Migori na Eldoret, Polisi waliripotiwa kushindwa kujua nini cha kufanya baada ya vijana kwa maelfu kujitokeza mitaani katika barabara zote kuu wakipinga mauaji yanayoendelea nchini humo.

Katika maeneo ya Rift Valley makundi ya watu wenye mapanga, mikuki na marungu yameendelea kusababisha hofu kutokana na kuongezeka kwa idadi ya vifo ndani ya siku mbili zilizopita

Taarifa mhudumu wa chumba cha kuhifadhi maiti kwenye hospitali ya Moi mjini Nakuru, mji ulioathirika kwa mauaji yaliyoanza upya mwishoni mwa wiki iliyopita ilisema kuwa hadi kufikia jana, kulikuwa na miili ya watu 64 waliouawa iliyokuwa imefikishwa rasmi katika chumba hicho.

Katika miji ya Migori na Eldoret, Polisi waliripotiwa kushindwa kujua nini cha kufanya baada ya vijana kwa maelfu kujitokeza mitaani katika barabara zote kuu wakipinga mauaji yanayoendela nchini humo.

Makundi kutoka pande zinazopingana yamekuwa yakipambana kwa nguvu mjini Nakuru na mji jirani wa Naivasha, kwa kutumia silaha hizo za jadi. Tukio la hatari zaidi lililotokea juzi ni pale watu nane walipofariki dunia baada ya kufungiwa ndani ya nyumba yao na kuchomwa moto.

Pia imeripotiwa kuwa malori 13 mali ya watu binafsi yaliteketezwa kwa moto katika mji mmoja ulioko Magharibi mwa nchi hiyo.

Mchafuko hayo yaliyoanza mara baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Rais Disemba 27 mwaka huu yamechukua sura mpya ya ukabila, huku yakihusishwa na migogoro ya ardhi na tofauti za kipato zilizojitokeza kwa miaka mingi iliyopita, suala ambalo linapingwa na viongozi wa ODM ambao wanadai kuwa hiyo ni mbinu ya kupotosha ukweli inayotumiwa na Rais kibaki na wafuasi wake.

Idadi ya watu waliouawa tangu kuanza vurugu mpaka sasa inakadiriwa kufikia zaidi ya 800, na zaidi ya watu 300,000 kukimbia makazi yao kwenda kutafuta hifadhi kama wakimbizi nchini Uganda.


Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post
 |  TrackBack URI for this post

Comments

Got something to say?