FIFA yazipa klabu miezi sita kubadilika ama kuondolewa kwenye ligi
November 18, 2007
SHRIKISHO la Soka Dunia(FIFA) limetoa miezi sita kwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kuanzia kubadili mfumo wa uendeshaji wa klabu hizo na kushindwa kufanya hivyo itakuwa ni sawa na kujiondoa mwenye kwenye ligi.
Hayo yaliazimiwa jana mjini Bagamoyo wakati wa kufunga kozi ya siku tano ya utawala na uongozi iliyoandaliwa na Shirikisho hilo kwa viongozi wa klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Katika maazimio hayo, klabu zimetakiwa kutekeleza utawala bora katika klabu zao ikiwa ni pamoja na mgawanyo wa madaraka na si kiongozi mmoja kufanya shuguli zote za klabu, kutowaingilia makocha katika kazi zao, kuweka mipaka ya kazi, kutoa ushirikiano mzuri kwenye vyombo vya habari, kubadili katiba zao ziendane na zile za FIFA pamoja na TFF ikiwa ni pamoja na katibu kuwa wa kuajiriwa badala ya kuchaguliwa,
Pia zimetakiwa kuzingatia mafunzo waliyopewa ya jinsi ya kuongoza wanachama na wapenzi wa klabu zao, kuzingatia mipango bora ya klabu, jinsi ya kuandaa matukio mbali mbali na jinsi ya kutafuta masoko kwa kuwa mpira ni biashara.
Klabu hizo zimepewa muda hadi ifikapo Mei mwakani ziwe zimetekeleza masuala hayo na klabu ambayo haitatekeleza itaondolewa kwenye ligi.
Akizungumza wakati wa kufunga kozi hiyo ya siku tano iliyoanza Novemba 11 na kufikia kilele chake jana, Mkufunzi wa FIFA ambaye pia anasimamia mradi wa goal project kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati Ashfod Mamelod alisema anatarajia ifikapo mwezi Mei mwakani klabu zote zitakuwa zimetekeleza maazimio hayo na kuzitaka klabu nyingine ziige mfano wa Simba na Yanga kwa kuweka rasilimali za klabu.
“Kati ya nchi 10 zilizochaguliwa kutolewa kozi hii Tanzania ni moja wapo, hamjiulizi ni kwa nini kozi hii imekuja Tanzania?,”alisema Mamelod kwa kuuliza na kuongeza, “Imekuja Tanzania kwa sababu si kwamba Tenga amegeuka, ni kwa sababu soka la Tanzania kwa sasa limepanda tofauti na siku za nyuma, nilipokuja kwenye uchaguzi mwaka 2004 niliona jinsi watu walivyokuwa wamechoshwa na uendeshaji wa soka la wakati ule nilijua ni lazima litabadilika kwa sababu mlitaka mabadiliko,”alisema.
Naye Naibu Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Joel Bendera, akizungumza wakati wa kufunga kozi hiyo aliwataka viongozi hao wa klabu kubadilika kwa kuzingatia mambo waliyojifunza na kuyatekeleza wawe na mwamko mpya wa kujadili kuzungumzia maendeleo ya mpira wa miguu badala ya kupoteza muda mwingi kuzungumzia na kutatua migogoro yao.
“Watu wa Simba na Yanga nimewapiga marufuku kuja ofisini kwangu kutatua migogoro yao, nashangaa wengine wakiwa na migogoro wanataka serikali ingilie kati tuingilie nini nimewaambia wazi kabisa sitaki kuwaona wengine niliwafukuza.
“Mbadilike jamani lazima viongozi wa klabu muwe na malengo ya kuendeleza mpira wa Tanzania kwa kuwa na programu mbali mbali za kuwaendeleza wachezaji wetu ili waweze kukuza vipaji vyao ili waje kuuzika nchi za nje,”alisisitiza.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya viongozi wa klabu za Ligi Kuu walikiri kuwa na mapungufu katika uongozi wao na kwamba kozi hiyo ya FIFA imewatoa matongotongo na kuwafungua upeo katika masuala mazima ya uongozi.
Mwenyekiti wa Yanga, Iman Madega alisema “Kozi ni nzuri nimebaini kuna udhaifu mkubwa katika uendeshaji, nitajitaidi katiba ya Yanga iendane na ya FIFA na TFF, nimefahamu jinsi ya kuongoza wanachama wangu, masuala mazima ya mgawanyo wa kazi sio utaratibu uliopo sasa mwenyekiti ndio anafanya kazi zote,”alisema Madega.
“Ukweli na wala sio jambo la kuficha benchi la ufundi huwa tunaliingilia lakini mambo hayo kwa Yanga sasa yamekwisha. Tutazingatia kufika mahali kwa wakati kama tulivyofundishwa, suala zima la kutafuta masoko mpira ni biashara na tutatengeneza uhusiano mzuri na wanachama na mashabiki wetu kuvutia wadhamini,.
“Kozi hii ni changamoto kubwa kwangu kwa kuwa niliamini vitu vingi najua kumbe sijui nilikuwa najidanganya nimefungua kurasa mpya nitahakikisha naibadilisha Yanga kwa kiasi kikubwa,”alisisitiza Madega.
Naye Rais wa Moro United, Ismail Aden Rage alisema “Klabu zote zilifanya presentation (kutoa taarifa zao) zote zinamapungufu,”alisema Rage.
“Naweza kusema kozi hii ni kiti moto kwa kuwa kumekuwa na uwazi zaidi makocha wameweka wazi mbele yetu kuwa wanaingiliwa kupanga kikosi cha kucheza kila mtu kaelezwa mapungufu yake. Ni kiti moto kati ya FIFA, Klabu na Makocha, tumepewa muda kurekebisha mfumo mzima wa uendeshaji na tumetakiwa tuwe na chama ambacho ni muungano wa klabu za ligi kuu,”alisema rais huyo wa Moro United.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Simba Omary Gumbo alisema “Nitahakikisha Simba inabadilika kwa kiasi kikubwa, ni lazima tufanye mabadiliko kama tukifuata maagizo hayo ya FIFA kwa muda wa miezi sita tutafaidika sana,”alisema Gumbo.
Naye Katibu wa Moro United Juma Simba alisema “Kozi hii imesaidia upeo wa viongozi kutanuka, kila kiongozi kajua mipaka yake, ni wazi viongozi tunamatatizo hasa inapotokea timu inafungwa hatuwasaidii makocha badala yake tunashirikiana na wanachama kuwabebesha mzigo usiostahili makocha na wachezaji,”alisema Simba.

