Fidel Castro Rais aliyenusurika kuuawa mara 638
February 27, 2008
FIDEL Castro, mwana mapinduzi aliyeiongoza Cuba kwa miaka 49, na kung’ang’ania kubaki madarakani hata afya ilipoanza kuwa mbaya miaka 10 iliyopita hatimaye ameachia ngazi.
Katika taarifa yake ya kujiuzulu, Castro (81), ambaye mwaka jana daktari wake, Eugenio Selman, alisema hakuwa na matatizo ya kiafya na ataishi kufikia umri wa miaka 140, amesema hawezi tena kuongoza nchi kwa vile hali yake si nzuri.
Mwana mapinduzi huyu ambaye wakati wa utawala wake hakuelewana na Marekani, alisema: “Ninachotaka ni kubaki kuwa askari wa mapambano ya kifikra… na labda sauti yangu itasikika.” Kauli hii imetafsiriwa kuwa ijapokuwa hayupo madarakani, lakini atabaki kuwa na sauti ya uamuzi.
Kinachosubiriwa sasa ni kuona je, Cuba itabadilika na kujiunga na wimbi linalovuma duniani kote la utawala wa kidemokrasia na watu kuwa na haki ya kuikosoa na kuipinga serikali yao? Hivi sasa nchini Cuba anayeipinga serikali anaonekana msaliti na mhaini.
Castro aliyekuwa madarakani kwa kipindi kirefu kuliko kiongozi yeyote duniani, alitaka kugombea uongozi kwa muhula mwingine. Lakini hali ilipokuwa mbaya, alimkabidhi madaraka mdogo wake, Raul Castro (76) ambaye ni mmoja wa makamu wa rais sita. Raul amekuwa Waziri wa Ulinzi toka mwaka 1959 na amekuwa akikaimu nafasi ya urais tangu afya ya kaka yake ilipozidi kuwa mbaya.
Castro amekuwa akionekana na sura tafauti nchini Cuba na nje kwa kutegemea mtazamo wa mtu au kikundi. Wapo wanaomuona mwana mapinduzi shujaa aliyeipenda nchi yake na wapo wanaomuona mtu katili aliyetawala kwa mkono wa chuma.
Castro alikuwa rafiki mkubwa wa baadhi ya nchi zinazoendelea, hasa zinazofuata siasa za kisoshalisti. Lakini kung’angania madaraka kwa miaka 49, hata alipokuwa anaumwa, na kumwachia uongozi wa nchi mdogo wake, hakutoi sura nzuri ya utawala bora.
Vile vile unapoona maelfu ya watu wanakimbia nchi yao na kuwa wakimbizi nchi za nje, lazima ukubali ukweli kwamba uongozi wa nchi yao una matatizo.
Hivi sasa zaidi ya Wacuba milioni 1.2 wameihama nchi yao, na zaidi ya robo tatu wanaishi Marekani. Cuba ina watu wapato milioni 12 na hii ni kusema asilimia 10 ya Wacuba wamechukua ukimbizi nje ya nchi yao.
Miongoni mwa waliomkimbia ni dada zake, watoto na wana wa familia zake na wote wanasema kilichowakimbiza sio shida za maisha, bali udikteta wa Castro wa kuonea watu.
Haiwezekani maelfu ya watu, wakiwemo wazee, wanawake, watoto na na watu wenye ulemavu, kujitosa katika bahari iliyojaa papa wakali katika boti ndogo ndogo na ngalawa kutaka kukimbia Cuba. Hata mamia walipokufa baharini, mamia zaidi waliona bora wakafe majini kuliko kuishi Cuba. Haiwezekani wote hawa walikuwa wendawazimu.
Lakini pia ni ukweli kwamba Wamarekani, miongoni mwa sababu zilizosababisha kumchukia Castro na kufanya kila njama za kumpindua na majaribio kadha ya kumuua, ni kutokana na kupoteza biashara, mashamba yao makubwa ya miwa na viwanda kutaifishwa. Hivi ndivyo Wamerakani wanavyokuwa pale wanapopoteza maslahi yao au wanapotaka kupata utajiri wa nchi, kama dhahabu au mafuta.
Kwa kawaida, madikteta hata wanapoacha uongozi bado hutaka kuitia nchi shemere na kulazimisha fikra na maamuzi yao yakubaliwe. Kauli ya Castro ya kutaka sauti yake iendelee kusikilizwa inaonyesha anataka kuendelea kuiongoza Cuba kupitia mikono ya mdogo wake.
Siku tatu tu baada ya kujiuzulu, Castro ambaye anasifika kwa hotuba na maandishi makali, alimjibu Rais George Bush wa Marekani aliyesema wakati umefika kwa Cuba, baada ya kuondoka Castro madarakani kubadilika.
Katika makala yake kwenye gazeti la serikali (chama) la Grandma, Castro ambaye hajaonekana hadharani toka Julai, mwaka 2006 alisema, Marekani ndiyo inayofaa kubadilika kwanza kwa kuiondolea Cuba vikwazo vya kiuchumi iliyoiwekea kwa zaidi ya miongo minne sasa.
Castro alipokuwa kijana alichukia ufalme na udikteta na ndiyo maana aliamua kuongoza mapinduzi ya nchi yake. Lakini tokea kushika hatamu ya uongozi mpaka alipostaafu, alitawala kwa mkono wa chuma na alikataa upinzani wa aina yoyote ile. Hata wale waliokuwa karibu naye walipotofautiana naye, aliwaua au kuwasweka gerezani na kuwatesa.
Fidel Alejandro Castro Ruz, alizaliwa katika familia ya matajiri katika shamba la sukari na baada ya kupata masomo ya awali kasinani, alichukua masomo ya sheria na kufungua ofisi yake ya uwakili.
Alisaidia sana watu masikini, na alijiunga na chama kilichokuwa kinapigania mageuzi cha Cuban People’s Party. Alipokuwa anataka kugombea ubunge mwaka 1952, Jenerali Fulgincio Batista aliipindua serikali na kufuta uchaguzi.
Castro kwanza aliyapinga mapinduzi mahakamani na alipoona hakuna mafanikio, aliunda jeshi la waaasi na jaribio lake la kufanya mapinduzi halikufanikiwa.
Alikamatwa na kuwekwa jela mpaka mwaka 1955 na alipotoka kwa msamaha wa Batista, alikwenda Mexico na kuunda kundi lililoipinga serikali lililojulikana kama Vuguvugu la Julai 26. Huko ndiko alikokutana na mwanamapinduzi maarufu, Ernesto ‘Che’ Guevara.
Katika mwaka 1956, kundi hilo liliivamia kambi ya Moncada, lakini walishindwa na wapiganaji wengi waliuawa, lakini Castro na Raul walinusurika na kuishia kufungwa, labda kutokana na umaarufu wa familia yao ya kitajiri.
Alipotoka jela, Castro aliendelea na mpango wake wa kufanya mapinduzi na baada ya mapambano ya miaka mitatu, akiwa na wenzake, waliingia Havana Januari 8, 1959 na kuchukua uongozi wa nchi, na haikuchukua muda akakorofishana na Rais Dwight Eisenhower wa Marekani ambaye aliapa kuiangusha Serikali ya Castro, hata kwa kutumia nguvu.
Baada ya kufa Eisenhower, marais wengine nane waliofuata (John Kennedy, Lyndon Johnson, Richard Nixon, Gerald Ford, Jimmy Carter, Ronald Reagan, George Bush (mkubwa) na Bill Clinton), wote walitaka kumng’oa Castro madarakani au kumuua, lakini nao wakashindwa. Na hata huyu wa sasa, George Bush, naye alihangaika bila mafanikio.
Kwa wana mapinduzi na wasoshalisti duniani, Castro alikuwa mtu mzuri, lakini nchini Cuba aliangaliwa vingine kutokana na misimamo yake mikali ya kukataa kukosolewa, na watu wachache tu kuwa ndio waliokuwa na kauli za kuamua nchi yao ielekee wapi.
Cuba imezisaidia sana nchi za Afrika kwa kutuma mamia ya madaktari mabingwa kusaidia sekta ya afya, na hivi karibuni tu ilipeleka madaktari 100 Botswana.
Cuba pia imesaidia sana harakati za ukombozi barani Afrika na miongoni mwa mchango wake mkubwa ni kupeleka majeshi katika vita vya ukombozi nchini Angola na kusaidia majeshi ya Ethiopia katika vita vya Ogaden na Somalia.
Lakini mtu aliyeshiriki vizuri katika vita vya ukombozi vya Angola na rafiki yake wa karibu sana, Jenerali Arnaldo Ochoa, naye alijiunga katika orodha ndefu ya watu waliouliwa na na Castro pale alipotwangwa risasi hadharani Julai 13, 1989 kwa kudaiwa ni msaliti na fisadi.
Kitendo kile kiliwapelekea Wacuba wengi kuamini hakuna mtu ambaye alikuwa salama nchini Cuba wakati wa utawala wa Castro.
Kwa upande mwengine, Castro hakuwa mtu aliyependa kujikomba, lakini watu wake wa karibu walimpa kila aina ya siasa kama vile ni “Mungu mdogo”. Mpaka leo hakuna jengo, wala barabara au taasisi iliyopewa jina la Fidel Castro na pia amekataa masanamu yake kujengwa nchini Cuba kama viongozi wengine wa kisoshalisti dunaini wanavyohusudu.
Castro alisimamia vizuri sera za kiuchumi nchini mwake na ugawaji wa ardhi kwa wakulima, lakini baadaye viongozi ndio waliofaidika kwa kumiliki maeneo makubwa ya mashamba.
Sekta za elimu na afya pia zimepata mafanikio mazuri, ijapokuwa wengi wanaamini takwimu zinazotolewa na serikali za mafanikio ya sekta hizi huwa zimetiwa chumvi.
Fabian Escalante, ambaye kwa zaidi ya miaka 30 amekuwa kiongozi wa ulinzi wa Castro, amesema rekodi alizokuwa nazo ni kwamba, Castro amenusurika kuuawa mara 638.
Majaribio haya ni pamoja na yale ya Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA), Wacuba wanaoishi uhamishoni na waliopo nje ya nchi.
Majaribio ya kumuua ni ya aina mbalimbali; kwa kumripua bomu, kumtwanga risasi, kumpiga sindano za sumu na kumtilia sumu katika chakula au kinywaji na kuweka sumu katika nguo zake na tumbaku aliyokuwa akivua.
Miongoni mwa waliofanya majaribo ya kumuua na kutofanikiwa ni mpenzi wake, Marita Lorenz, ambaye alitaka kumpa vidonge vya sumu wakiwa chumbani, na Castro alipogundua alimuua.
Castro aliwahi kusema kama kunusurika kuuaa mara nyingi kungelikuwa tukio la Olimpiki, basi angelibeba kwa urahisi medali ya dhahabu na kama mashindano mengine ya kuua watu nayo ni tukio la Olimpiki, basi mabeberu wa Marekani wangenyakua medali ya dhahabu.
Hata hivyo, Castro hazungumzii mamia ya watu aliowapiga risasi au kuwaua kwa mateso nchini Cuba. Upo wakati Cuba, baada ya kusambaratika kwa Umoja wa Nchi za Kisoviet mwaka 1991, ilikuwa imefilisika. Zaidi ya asilimia 85 ya soko la bidhaa zake, hasa sukari, likatoweka na kila bidhaa ilikuwa shida kupatikana.
Viwanda 118 vya sukari na chuma vilifungwa, lakini juu ya shida zote hizo, Castro ameweza kubakia madarakani na kilichomsaidia ni kupeleka maelfu ya madaktari Venezuela kwa kubadilishana na mafuta mwaka 2005.
Baada ya hapo, Cuba ikaanzisha uhusiano wa kibiashara na nchi moja moja za Ulaya, lakini si na Umoja wa Ulaya.
Katika miaka ya mwisho ya utawala wake, Castro ambaye haamini Mungu, amekuwa akiruhusu watu kuabudu, jambo ambalo lilikuwa ni uhaini miaka ya nyuma.
Sasa Castro amejiuzulu na mdogo wake Raul ambaye katika miaka ya karibuni amekuwa akigusia umuhimu wa kila mwananchi kutoa mawazo yake bila ya woga na kuomba yaheshimiwe, ameshika hatamu.
Kinachosubiriwa ni kuona watu gani watakuwemo katika Serikali ya Raul. Kwa muda mrefu Serikali ya Castro imekuwa na wazee wa miaka 70 na kuendelea, na wapo mawaziri wachache wenye umri wa chini ya miaka 60.
Ni tabu kutabiri nini kitatokea Cuba baada ya Fidel Castro kuachia ngazi ya uongozi, lakini zipo ishara za kuwepo mabadiliko, lakini kinachongojewa ni kasi ya mabadiliko.
Zama za Castro sasa ni sehemu ya historia, ijapokuwa amesema atategemea kauli zake kusikika, lakini kama wasemavyo Waswahili, siku zote komba wapya huwa na msitu mpya ijapokuwa mara moja moja huzuru ule wa zamani.
Tungoje na tuone. Lakini kwa vyovyote Fidel Castro atakumbukwa kwa mengi mazuri na mabaya nchini Cuba na nje.

