Endeleeni kuwafichua mafisadi - Kawawa
April 18, 2008
MAKAMU Mwenyekiti Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rashidi Kawawa, amewataka Watanzania kuwa wawazi na kuendelea kuwafichua mafisadi ili kulinda maslahi ya nchi.
Alitoa wito huo Dar es Salaam jana kwenye uzinduzi wa kitabu kiitwacho ‘CCM na Mustakabali wa Nchi Yetu’, kilichoandikwa na Makwaia wa Kuhenga.
“Hatupendi kusikia jambo la ulimbikizaji wa mali, wanaofahamika watajwe hadharani na waeleze fedha hizo wamezipatapataje na wamezipata wapi,” alisema Kawawa.
Alisema kuwapo kwa mafisadi ndani ya chama tawala ni jambo la hatari ambalo linaweza kukiweka chama hicho katika wakati mgumu.
Amewataka wana CCM kutambua kuwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, hakuwa mtu mwenye tamaa ya kujilimbikizia mali, hivyo changamoto hiyo haina budi kuzingatiwa.
“Mimi sikuwa na mabilioni ya fedha, hivi ningeyapata wapi? Mwalimu Nyerere hakuwa mtu mwenye tamaa, hata hakujilimbikizia mali, hii iwe ni changamoto kwa wana CCM,” alisema. Akizungumzia uzinduzi wa kitabu hicho, Kawawa alisema ni vema viongozi wa CCM wakatambua mchango wa mtunzi wa kitabu hicho, wakapokea mawazo yake na kuyafanyia kazi.
“Yote yaliyoandikwa katika kitabu hiki ni changamoto kwa viongozi wa chama chetu, tunapojadili mambo mazito kama yaliyomo katika kitabu hiki, tunatakiwa kuwa watulivu na wenye kutanguliza mbele uzalendo na utaifa wetu,” alisema Kawawa
Alisema mtunzi huyo amekikosoa chama na Serikali zake, na kwamba kukosolewa huko ni sehemu ya wana-CCM kushiriki mjadala huo, ama kwa kukubali kukosolewa, au kutokubali kwa nguvu za hoja ambazo zitaendeleza ustawi wa chama na taifa.
“Mwongozo wa CCM wa mwaka 1981 ulitamka bayana kwamba kujikosoa na kukosoana ni silaha ya mapinduzi, alichofanya Makwaia wa Kuhenga ni kukikosoa chama na Serikali yake, hii ni changamoto ya kushiriki mjadala utakaoelekezwa kuimarisha ujenzi wa taifa letu,” alisema Kawawa.
Kwa upande wake, Makwaia alisema ameamua kuandika kitabu hicho kwa kuwa chama kimepoteza mwelekeo, hali ambayo inasababisha viongozi kukiuka maadili.
“Mimi ni mwandishi wa habari, kazi ya mwandishi ni kuandika rasimu ya historia ya kila siku, kwa hiyo mwandishi ni lazima atambue tuko wapi na tunaelekea wapi, awamu zote nimeziona, lakini tunakoelekea sasa siko.
“Mabadiliko haya yanajionyesha wazi, mfano baadhi ya wanachama wa vyama pinzani wakihamia CCM, kinachofuata ni kupewa madaraka, kwa hiyo CCM ya sasa ni kidikiro, yaani sehemu ya kurukia sehemu fulani,” alisema Makwaia.
Aliongeza kuwa kuporomoka kwa maadili ya chama hicho kumekuwa na mtazamo mbaya unaowafanya baadhi ya wanachama kuhangaika na kutumia fedha nyingi ili kuingia kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).
Kitabu hicho kinajadili masuala ya msingi 17. Kati ya hayo, masuala 13 yanatajwa kwa njia ya maswali likiwamo swali la Madaraka Nyerere linalouliza Azimio la Arusha lina tatizo gani? Kutoka Dodoma, Pendo Mangala, anaripoti kuwa umoja wa vyama vya siasa mkoani humo unatarajia kufanya maandamano yenye lengo la kumtaka Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, asiingie bungeni.
Umoja huo umesema umekerwa na kauli ya Chenge, ya kwamba fedha kwenye akaunti yake nchini Uingereza, ni vijisenti tu.
Msimamo wa umoja huo ulitolewa jana wakati wa kikao cha pamoja kwa ajili ya kutoa tamko kwa waandishi wa habari
Mwenyekiti wa umoja huo, Kayumbo Kabutali, alisema kuwa hawaoni mantiki kwa Chenge kuonyesha dharau, wakati fedha anazotuhumiwa kujilimbikizia, ni mali ya wananchi.
Alisema fedha alizonazo waziri huyo ni nyingi, na kwamba haiwezekani akamiliki ukwasi huo ndani ya lindi kubwa la umasikini linalowakabili wananchi. Umoja huo ulitoa wito kwa Rais Jakaya Kikweye kumchukulia hatua, kwa kumwondoa kwenye orodha ya mawaziri.
Maandamano hayo yamepangwa kufanyika Aprili 21, mwaka huu. Yataanzia Viwanja vya Mwalimu Nyerere (Nyerere Square) na kumalizikia katika viwanja vya Bunge
Alisema maandamano yataanzia katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere, kama sehemu ya kumuenzi kiongozi huyo mwadilifu aliyekuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya ufisadi.

