Cheche za mabadiliko ziwafikie Watendaji wabovu

February 25, 2008

BILA ya kuwa na uongozi ulio imara katika serikali za mitaa ni dhahiri kuwa hali ya uchumi wa taifa hili itaendelea kuwa na mwelekeo usioridhisha.

Maisha ya mtanzania kwa kiasi kikubwa yatajengwa na utawala bora kuanzia katika ngazi za juu za uongozi.

Na kwa kulitambua hilo kuna kila dalili kuwa rais ameona jinsi utendaji ulivyo mbovu katika baraza lake la mawaziri kiasi cha kuamua kulivunja kwa nia ya kuboresha utendaji wake.

Hata hivyo bado kuna matatizo makubwa kiutendaji katika ngazi hii ya serikali za mitaa.

Labda hali hii ilichangiwa na mazoea yaliyokuwa yamejengeka miongoni mwa watendaji hawa kutokana na kuamini kuwa utamaduni ni kujichukulia chako mapema bila kujali miiko ya uongozi na nafasi zao za kazi.

Malalamiko mengi yamekuwa yakitolewa na wananchi juu ya tabia mbaya inayofanywa na watendaji katika serikali za mitaa hadi baadhi yao kupendekeza kuwa kuna haja ya kuangalia namna ya kuchagua watendaji hawa kwa kuangalia vigezo mbalimbali kama vile elimu.

Baadhi ya watendaji wa halmashauri hizi kwa ujumla kwa kiasi kikubwa wanazorotesha maendeleo ya nchi.

Kwa kulitambua hili, aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ambaye sasa ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliwahi kuwakemea mabosi hawa wanaosimamia hovyo fedha za serikali, wengi wao kwa nia ya kujinufaisha wao wenyewe.

Akifungua Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa,mwaka 2006, Waziri Pinda alitamka bayana kuwa:

“Nidhamu ya matumizi ya fedha si ya kiwango cha kuridhisha. Halmashauri zinapata fedha nyingi kutoka Vyanzo mbalimbali vya mapato kama vile: Mfuko wa Pamoja (Basket Fund), TASAF, MMEM, MMES, Mfuko wa Barabara (Road Fund). Fedha hizi hazitumiki vizuri katika baadhi ya Halmashauri.”

Baadhi ya tuhuma alizoziongelea Pinda, ni pamoja na baadhi ya watumishi na viongozi wa Halmashauri kuwa na makampuni ya uwakala wa kukusanya mapato na pia vitendo vya baadhi ya watumishi na viongozi kuwa na kampuni ambazo zinafanya biashara na Halmashauri wanazozitumikia, tabia ambayo ni kinyume na maadili ya utumishi wa umma na ya viongozi wa kisiasa.

Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa walitakiwa kuwa makini katika kutoa zabuni kwa kampuni mbalimbali ili mapungufu haya yasiendelee kujitokeza.

“Zaidi ya yote alisema kuwa serikali kwa upande wake haitasita kutoa adhabu kali kwa wahusika wote mara suala la namna hii litakapogundulika.”

Pamoja na mwongozo huo wa serikali, tabia za viongozi hawa bado zinatia mashaka hasa katika masuala ya udhibiti na usimamizi wa fedha.

Baadhi ya madiwani na watendaji wengine wa Halmashauri za wilaya, wanaendelea kufanya ndivyo sivyo.

Tatizo la madiwani kuendekeza maslahi binafsi badala ya yale ya wananchi na Halmashauri zao limekithiri pia katika utoaji wa tenda za ujenzi wa barabara za wilayani jambo linalolalamikiwa na baadhi ya makandarasi kuwa linakwenda kwa kujuana huku takrima ikichukua nafasi.

Tatizo jingine ni kuwepo kwa baadhi ya madiwani ambao hawajui mipaka yao ya utendaji kazi, jambo ambalo kwa kiasi kikubwa linarudisha nyuma maendeleo.

Ni wajibu wa serikali kuu na mamlaka husika kuonyesha dhamira ya wazi katika kuwaadabisha watendaji wabovu na si kuendelea kuwafumbia macho.

Hatua zinazoweza kuchukuliwa ni pamoja na kuweka bayana mipaka yao ya utendaji kazi ili ijulikane wazi wajibu wa kila mmoja na si kama hali ilivyo hivi sasa ambapo ni vigumu kuelewa majukumu ya Wenyeviti, Mameya na Watendaji.

Lakini pia kuna kundi la watendaji hawa hususani madiwani ambao hata vigezo vyao vya kuteuliwa kama viongozi wa kisiasa na kupewa madaraka makubwa katika maamuzi na usimamizi wa fedha nyingi zinazotolewa na serikali kuu, imeonyesha si tija katika kuleta maendeleo.

Kama inavyojulikana,vigezo vya kuwachagua madiwani haviangalii elimu yao kama ni moja ya vigezo muhimu katika kuwania nafasi hizo.

Hali hii kwa kiasi kikubwa husababisha wale wanaopendwa na wananchi wao kuchaguliwa kushika wadhifa huu na hivyo kupewa mamlaka makubwa ya usimamizi na pia kuwa na ushawishi mkubwa katika maamuzi ya kutoa zabuni na matumizi ya serikali za mitaa kwa ujumla.

Ili kuleta maendeleo ya kweli katika usimamizi wa fedha nyingi zinazopelekwa katika serikali za mitaa, kuna haja ya kuangalia mustakabali mzima hasa katika chaguzi zenyewe na yupi mwenye mamlaka ya kufanya maamuzi mazito yanayohusiana na malipo.

Kama ilivyo mabadiliko katika serikali kuu basi tuzidhibiti serikali hizi za mitaa ili maendeleo ya kweli yawafikie walengwa.

Haitakuwa busara kama mafisadi hawa wataendelea kuwapo huku nchi ikiwa inapita katika kipindi hiki kigumu cha mabadiliko.

Kuna mikakati mingi tu ambayo serikali imejiwekea ili kuhakikisha kuwa kunakuwepo na mabadiliko katika maisha ya Mtanzania.

Mikakati hiyo ambayo yote hutelekezwa katika serikali za mitaa ni pamoja na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 ambayo inahusisha programu mbalimbali ikiwemo Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Tanzania (MKUKUTA), ambayo kwa hakika haitafanikiwa kama aina ya viongozi waliopo hawatabadilika au kuondoshwa kabisa.

Cheche za mabadiliko yaliyofanywa na rais katika kuwawajibisha waovu, mafisadi katika Serikali Kuu wasiojali maisha ya wananchi na kuweka mbele maslahi yao liwafikie na hawa wajanja wachache waliopo katika serikali za mitaa.

Kuna madiwani ambao wanasainishwa kiujanjaujanja mikataba ya ujenzi wa barabara na kuwahadaa wasimamizi hawa serikali kwa takrima.

Hawa nao ni mafisadi ambao wanaonekana kama ni wadogo wadogo lakini ni hatari kwa taifa.

Serikali itathibitisha kuwa ina nia thabiti ya kurekebisha hali ya mambo kwa kusafisha baadhi ya madiwani ambao wamekuwa wakilalamikiwa na wananchi kwa utendaji wao mbovu wa kazi usiokuwa na tija kwa taifa.

Wakati wa mapinduzi ni sasa, tunahitaji maendeleo ya kweli.

Jonas Songora ni mwandishi wa makala wa gazeti la Mwananchi.


Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post
 |  TrackBack URI for this post

Comments

Got something to say?