Chacha wangwe anavyocheza ngoma ya mafisadi
April 3, 2008
NIMESOMA habari iliyoandikwa katika gazeti moja la kila siku (si Mtanzania), la Jumanne ya Machi 25, mwaka huu, yenye kichwa cha habari: “Ufisadi wadaiwa kuathiri vyama vya siasa.”
Habari hiyo imetokana na mahojiano ya mwandishi wa habari hiyo na Mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kama alivyomwelezea mwandishi wa habari husika.
Kwa hakika, baada ya kuisoma nilipata mshtuko. Lakini nilikumbuka kwamba katika falsafa ya fasihi, moja ya kigezo cha kufikia hukumu, ni pamoja na kutazama historia ya tabia ya mhusika.
Hapo ilibidi nijikumbushe kidogo historia ya kauli za Wangwe, za huko nyuma. Nikakumbuka kuwa moja ya udhaifu mkubwa alionao Wangwe, kuanzia bungeni na hata katika siasa za majukwaani, ni muumini wa siasa za uchochezi, na katika kutekeleza hilo, huwa hasiti kutumia ulaghai.
Sote tunakumbuka namna alivyowalaghai Watanzania kwamba Serikali ilivunja Katiba ya nchi kwa hatua yake ya kupeleka majeshi Comoro, akidai kwamba ilihitajika kwanza Bunge liridhie, ilhali ukweli ni kwamba alichonukuu Wangwe, kilikuwa uamuzi wa nchi kuingia vitani dhidi ya nchi nyingine, na si uamuzi wa nchi kushiriki oparesheni za kijeshi za kikanda, Umoja wa Afrika na au Umoja wa Mataifa.
Hata hivyo, Wangwe kwa kutojua au kwa dhamira ya kupotosha umma, aliamua kulipuka kwenye vyombo vya habari, akisema asichokijua na hatimaye watu makini wakaanza kumbeza yeye na hata chama chake kilichompa uongozi huo.
Ulaghai wa Wangwe haukuishia hapo. Katika mikutano yake ya oparesheni ya Tabata Dampo, alinukuliwa na gazeti moja la kila siku pia (si hili), akidai kwamba analala na wahanga wa kuvunjiwa nyumba, ilhali wananchi wakikana katika vyombo vya habari kuwa Wangwe hakuwa amewahi kulala hata siku moja pale Tabata Dampo, kama anavyodai mwenyewe, ishara ya mshikamano.
Kwa kifupi ni ukweli kwamba kwa muda wote, pamoja na makeke mengi ya mbunge huyo wa Tarime, ameendelea kuonekana kama mwansiasa wa eneo fulani (local politician), ambaye kwa kipindi cha hivi karibuni, ameanza bila mafanikio harakati za kujitambulisha kama mmoja wa wanasiasa wenye hadhi ya kitaifa.
Anatamani kuwa kama walivyo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu wake, Dk. Willbrod Slaa na na Kabwe Zitto na kadhalika, na au walivyo kina Maalim Seif Sharrif Hamad na Profesa Haruna Lipumba wa CUF.
Hali hiyo, inamfanya ajikute akitamka chochote walau asikike hali inayozidi kubainisha wazi uwezo mdogo na muono finyu alionao katika dunia ya wachambuzi wa masuala ya siasa.
Ni katika muktadha huo, haiyumkiniki kusoma maelezo ya kiongozi wa aina hiyo na kuyaamini. Na lakini pia, ni wazi sasa kwamba Wangwe amejiweka katika mazingira ambayo kauli, ahadi na maelezo anayoyatoa, yashindwe kuaminika kwa yeyote kabla ya kuyafanyia uchunguzi wa kina.
Ni kiongozi asiyetambua thamani ya kauli anazotoa, na hivyo kupunguza umakini wa kauli zake kwa kuwa zinaweza kumtoka bila hata ya kuzifanyia utafiti tofauti na ilivyo kwa wabunge wenzake, mfano Kabwe, Dk Slaa na wengine katika kambi ya upinzani.
Kwa mfano, kauli ya hivi karibuni ya Wangwe, ya kwamba ndani ya chama chake cha Chadema kuna matumizi mabaya ya fedha, ambayo ni sawa na ufisadi, haikuniingia moja kwa moja akilini kutokana, kwanza kwa wakati anaozungumzia suala lenyewe, lakini zaidi, rekodi ya mwanasiasa huyo ya kusema asichokijua, na au kulaghai wa umma kwa taarifa potofu, ilimradi tu afikie malengo yake kisiasa.
Binafsi, nilidhani kama kiongozi wa juu wa Chadema angefanya utafiti kwanza kwa hilo analolisema, ili kubaini athari zake kwa chama chake kiasisa.
Katika muktadha wa nyakati, ni wazi kuwa Chadema kimeweza kujitofautisha na Chama Tawala (CCM) mbele ya umma wa Watanzania, kwa namna viongozi wake walivyosimama kidete kuanzisha vuguvugu la kutaka umma usimamie rasilimali za nchi, ikiwa ni pamoja na kuzindua kampeni za vita dhidi ya ufisadi kwa matukio kadhaa bungeni, lakini mahsusi ile ya Kabwe
na madini, ikifuatiwa na ile ya Dk Slaa na ufisadi wa EPA, ambazo zote zimezaa matunda kwa Taifa, na tayari historia imekwishawaandika wapambanaji hao.
Hata hivyo, baada ya mafisadi kuona hatari ya Chadema pamoja na baadhi ya wabunge wa CCM na wanaharakati wengine nchini, wamezindua mkakati wa ‘bora tuchafuke wote,’ na sasa kwa makusudi mazima, wamekuwa wakitoa tuhuma za uzushi kuhusu wapambanaji hao, kwa kuwatumia wanasiasa dhaifu kama Wangwe, likiwamo hili la Mbowe kuifilisi NSSF, ilhali Mkurugenzi wa NSSF mwenyewe akishangaa uamuzi wa mafisadi hao kuita mkopo kuwa ufisadi.
Aidha, Mkurugenzi wa NSSF, anashangaa mafisadi hao wanaotafuta mlango wa kutokea, wametoa wapi takwimu hizo, huku akikiri kwamba kama Mkuu wa NSSF, hajui ni kiasi gani wanaidai Mbowe Hotels, licha ya kufahamu kuwa Mbowe alikopa milioni 15, na amekwisha lipa deni lake pamoja na riba yake kwa kiasi cha Sh milioni 75.
Ninachojaribu kuweka wazi hapa ni kwamba upo mkakati wa mafisadi kuwachafua wapambanaji makini katika nchi hii, pamoja na asasi makini kama Chadema, ili kuwakatisha tamaa Watanzania ya kwamba mabadiliko ya kweli hasa yanawezekana.
Kwa hakika, huo ni mkakati waliouchagua baada ya kuona ule wa kujisafisha umegonga mwamba. Wananchi wameshtuka.
Ni katika mazingira hayo, kwa Mtanzania makini, anaweza kuweka kauli ya Wangwe kwenye kapu moja la malengo ya mafisadi kutaka kuwachanganya wananchi kwa mazingaombwe ya kuwachafua watu safi, na hata asasi safi kama Chadema.
Na huo ndio ulikuwa msingi wa mimi kuamua kufanya uchunguzi ili kubaini kama dhana iliyojengeka akilini mwangu kuhusu Wangwe ilikuwa sahihi au la! Baada ya uchunguzi wangu, nimebaini kwamba Chadema imekuwa ikiweka wazi matumizi yake ya fedha, kuanzia matumizi ya kawaida na hata ya kampeni za uchaguzi na za uendeshaji wa chama kwa mwaka mzima.
Taarifa za matumizi ya fedha wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge wa Kiteto iliwekwa wazi kwa wananchama wake, na jumla kuu ilifikia Sh milioni 59.7, ikiwa ni fedha za chama na michango ya viongozi, wabunge na wahisani wengine.
Lakini pia, taarifa za chama hicho zinaweka wazi kwamba gharama za Uchaguzi Mkuu 2005, ni Sh milioni 750, kwa kampeni za mgombea urais.
Taarifa zote hizo zipo wazi na zinapatikana hata kwenye tovuti ya Chadema, ya www.chadema.net. Je; kuna uwazi kupita huo katika vyama vyetu vya siasa nchini?
Mara ngapi CCM kimekataa kutangaza matumizi yake wakati wa kampeni za uchaguzi? Kwa nini basi Wangwe anashindwa kuuona ukweli huo, tena kwa nafasi yake ya Makamu wa Mwenyekiti? Aibu sana!
Ni ukweli pia kwamba kila chama cha siasa nchini, hutakiwa na sheria ya vyama vya siasa kuwasilisha matumizi ya ruzuku inayotolewa na Serikali kila mwaka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.
Je, ni lini Wangwe amewahi kuulizia taarifa hizo, walau basi kwa Msajili wa Vyama vya Siasa? Je; mpaka anakuwa Makamu Mwenyekiti wa chama makini kama Chadema, hajajua mambo madogo madogo tu kama haya?
Hivi Wangwe hajui pia kwamba ni wajibu wa Msajili wa Vyama vya Siasa kuweka wazi matumizi ya ruzuku inayotolewa kwa vyama vya siasa nchini?
Niwazi kuwa kama Makamu Mwenyekiti, Wangwe alipaswa kufahamu mifumo ya uendeshaji wa idara ya fedha katika Chadema, kwa kuwa siku zote, katika maelezo yote yanayohusu fedha za chama, imekuwa ikielezwa kuwa dira ya mapato na matumizi ya chama hupitishwa na kikao cha Baraza Kuu la Chama, kikao ambacho Wangwe ni mjumbe.
Lakini pia, kila kikao cha Kamati Kuu ya Chadema, taarifa ya fedha hutolewa na kujadiliwa, kikao ambacho pia Wangwe ni mjumbe. Je; kwa kusema kuna ufisadi katika matumizi ya fedha ndani ya chama chake, Wangwe anataka kutuambia yeye mwenyewe hakubaliani na maamuzi ya Baraza Kuu la Chama chake?
Nasema Baraza Kuu, na si Kamati Kuu, kwa kuwa tayari Wangwe ameshanukuliwa na vyombo vya habari akipinga maamuzi ya Kamati Kuu, kuridhia matumizi ya helkopta katika opareshani za siasa, ikiwa ni kama wiki moja tu, tangu Kamati Kuu ya chama hicho iketi jijini Dar es Salaam na kukubaliana na suala la matumizi ya helkopta.
Na katika mazingira ya kushangaza, chama hicho ingawa kimeendelea kutumia helkopta, kiasi cha hata CCM kuamua kuiga, chama hicho, kuonyesha namna kilivyo makina hakijawahi kumchukulia hatua yoyote kiongozi huyo.
Kama Kamati Kuu ya Chadema iliamua kumpuuza Wangwe, na au haina mamlaka ya kinidhamu dhidi ya Makamu Mwenyekiti, hilo ni suala jingine!
Ni wazi kwamba katika vyama vya siasa vya upinzani, Chadema ni moja ya vyama vinavyoongoza kwa kufanya matukio na oparesheni nyingi za kisiasa kwa upande wa Tanzania Bara.
Ni Chadema hiyo inayopata ruzuku ya karibu Sh milioni 65, lakini inayopeleka wilayani kwa ajili kuimarisha chama, zaidi ya Sh 12,000,000 kila mwezi.
Lakini pia ni Chadema hiyo hiyo inayoshindana vikali na CCM katika ulingo wa siasa, kwa kufanya matukio makubwa yenye kutikisa nchi kama kuendesha ziara mikoani, kiasi cha kuiacha CCM ikiwa hoi pamoja na chama hicho tawala kupatiwa ruzuku ya zaidi ya Sh bilioni 1.23 kila mwezi.
Kwa wapenda mageuzi nchini, tunauona uamuzi wa Wangwe, wa kukishambulia Chama chake, ni sawa na chokochoko zenye nia ya kutafuta njia ya kukipasua na kukimaliza kabisa Chadema kisiasa, kama ilivyotokea kwa NCCR Mageuzi miaka ya mwishoni mwa 1990.
Ni wazi kwamba hata kama Wangwe anaweza asiwe fisadi, lakini ni ukweli usiopingika kwamba anachokifanya ni utapeli, na zaidi anaendeleza mchezo wa ngoma ya kifisadi ili kukiangusha na kuikiangamiza Chadema.
Katika hili la sasa la Wangwe, nalazimika kukubaliana na kauli ya mwanasiasa mkongwe, Waziri wa TAMISEMI, Steven Wassira, kwamba anaendeleza mchezo wake wa utapeli wa kisiasa.
Ni muhimu kwa Wangwe kuachana na tabia ya ulaghai kwa Watanzania, ilhali ameshindwa hata kuongoza jimbo lake la Tarime. Kwa hakika, Wangwe ni adui wa maendeleo, apuuzwe.
Mwandishi wa makala haya amejitambulisha kwamba ni mwanaharakati, mwanachama wa Chadema na pia Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro. Anapatikana kwa Barua Pepe: asaid@yahoo.com
Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post | TrackBack URI for this post
Comments
Got something to say?

