CCM msukosuko Musoma
March 27, 2008
BAADHI ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), wanaojiandaa kwa ajili ya kikao chao kinachofanyika mwishoni mwa wiki huko Butiama, wamepata wakati mgumu mjini Musoma. Wajumbe hao ambao jana walianza kutembelea miradi ya maendeleo na kuona utekelezaji wa Ilani ya chama chao katika Jimbo la Musoma Mjini, walikumbana na upinzani wa wazi kutoka kwa wananchi waliokuwa wakipiga kelele za kudai kurejeshwa kwa fedha za EPA zilizofujwa kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Adha hiyo ilianza muda mfupi tu baada ya Naibu Meya wa Mji wa Musoma, Daudi Misango, kusimama kwa ajili ya kuanza kuwatambulisha wajumbe hao wa NEC waliokuwa wakiongozwa na Waziri Kiongozi wa zamani wa Zanzibar, Dk. Mohammed Gharib Bilal.
Aliposimama naibu meya huyo na kuwataka wananchi waliokuwa wamefurika katika viwanja vya Mkendo kuitikia kiitikio cha ‘CCM oyee!’ wananchi takriban wote walinyamaza na kuwaacha makada wachache wa chama hicho waliokuwa wamekaa mbele kuitikia kwa uchache.
Ukimya huo uliofuatiwa na kelele za ‘tunataka pesa za EPA kwanza’, kulisababisha Misango abuni mbinu mpya ya kuwalazimisha wananchi hao kuitikia salamu ile ya CCM oyee! Kwa kuwaita wachawi wale wote ambao walikuwa hawanyoshi mikono juu kuitikia salamu za chama hicho tawala.
“Mmm hapa naona kuna wachawi, tuanze tena; CCM oyeee,” alisema Misango ambaye alipigwa na butwaa, baada ya kuona umati mzima uliokuwa umesubiri mkutano huo kwa muda mrefu ukiwa kimya, hali iliyomlazimisha ateremke jukwaani mara moja.
Hali hiyo ilisababisha Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini, Vedastus Mathayo, ambaye pia ni mjumbe wa NEC Mkoa wa Mara, kupanda jukwaani ili aendelee na kazi ya kuwatambulisha wageni.
Mathayo wakati akitambulisha wajumbe wenzake, mmoja baada ya mwingine, alikumbana na tukio la ukimya wa wananchi hao wakati mjumbe mmoja wa NEC kutoka Zanzibar aliposimama na kusalimia kwa kusema: ‘Viatu vya mtoto mkubwa havai’.
Ukimya huo wa wananchi ulisababisha Mathayo kuwataka wajumbe hao wa NEC kutulia, kwa kusema wananchi wengi wa jimbo lake walikuwa hawajui Kiswahili cha Kizanzibari na ndiyo maana walishindwa kuitikia salamu za mjumbe aliyetumia usemi huo.
“Jamani nyie wageni wetu msishangae. Sisi huku Kiswahili hatukijui… nawaombeni wananchi kuwa makini kusikiliza, mjue kule Zanzibar wao wanasema skuli, sisi tunaita shule… wenzetu wanasema maji ya mfereji, sisi ya bomba, na huku tunasema sokoni, wao wanasema marikiti, hicho ni Kiswahili tu,” alisema Mathayo, kauli iliyofuatiwa na migumo na kuzomea kwa baadhi ya wananchi.
Alipoendelea na hotuba yake kwa kusema Ilani ya CCM katika jimbo hilo imetekelezwa kwa asilimia 80 na hivyo kufanya wananchi kuridhishwa na utendaji wa serikali na chama tawala, wananchi walianza kuondoka mmoja baada ya mwingine katika mkutano huo wa hadhara wakiguna na hivyo kuwaacha wana CCM waliokuwa wamevalia sare za kijani na njano za chama hicho kubakia uwanjani hapo.
Akihutubia mkutano huo baadaye, wakati watu wakiwa wameshapungua, Dk. Bilal aliipongeza serikali ya manispaa hiyo kwa kutekeleza ilani hiyo kwa asilimia 80.
Alisema hatua ya kufanyika kwa kikao cha NEC Butiama, kunatokana na maamuzi ya kikao hicho hicho ya kutaka kuona vikao vyake vikifanyika mkoa mmoja baada ya mwingine, huku Mara ikipewa nafasi ya kwanza.
Alisema pia mkutano huo unaotarajiwa kufanyika kwa siku mbili – Jumamosi na Jumapili ya wiki hii, unalenga kuleta umoja na mshikamano ndani ya chama na taifa kwa ujmla.
Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post | TrackBack URI for this post
Comments
Got something to say?

