Benki Kuu yabadili utaratibu wa kuuza amana

October 29, 2007

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imebadili utaratibu wake wa kuuza amana za serikali kutoka kipindi cha wiki hadi mwezi.

Uamuzi huo umetangazwa wiki moja iliyopita na BoT, ikiwa ni moja ya mabadiliko makubwa ya kiutendaji yaayoendelea kufanyika ndani ya BoT.

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, Naibu Gavana wa BoT, Juma Reli, alisema uamuzi huo unalenga kuipa uwezo serikali kufanya tathimini ya amana zake.

Reli alisema muda wa wiki mbili haukuwa ukiipa nafasi kubwa zaidi serikali kufanya tathimini ya kina kuhusu aina ya amana, ambazo inapaswa kuuza kwa ajili ya kila mwezi.

Naibu Gavana huyo aliongeza kwamba, mabadiliko hayo pia yataongeza ushindani kwa mabenki na wadau watakaotaka kununua amana hizo za serikali.

“Ni kweli tumebadili utaratibu wa kuuza amana za serikali, sasa hivi siyo kila wiki bali ni kwa mwezi,” alisema na kuongeza,

“Hii itaisidia serikali kufanya tathimini ya kina kuona amana zipi zinapaswa kuuzwa, lakini pia utaratibu utaongeza ushindani kwa wazabuni ambao watakuwa wakijianda kununua amana kwa mwezi,” alisema.

Kuhusu mwelekeo wa uchumi wa nchi, alisema hadi sasa ni mzuri ingawa umekuwa ukipata misukosuko kutokana na kupanda kwa gharama za mafuta katika soko la dunia.

Alisema kupada huko kwa bei ya mafuta ambako wiki iliyopita pipa moja ilifikia hadi dola 90, kumekuwa kukichangia mfumuko wa bei katika baadhi ya bidhaa.

Kuhusu kupanda thamani kwa shilingi dhidi ya dola, alisema sasa hivi ni msimu wa mauzo ya mazao nje ya nchi pamoja na kuweo ongezeko la fedha za misaa kutoka nje.

Alisema hali hiyo imefanya mahitaji ya shilingi kuwa makubwa kuliko kawaida hivyo kuongeza thamani yake.

Katika wiki iliyopita shilingi katika baadhi ya maduka ya kubadilishia fedha, ilionekana kuimarika na kufikia hadi sh 1,100 kwa dola moja kutoka sh 1,300 hadi 1,350