Bangusilo aliyewaponyoka watawala

February 27, 2008

MGENI anapokuja mara nyingi tunawatuma watoto waende kukamata jogoo ili tutengeneze kitoweo. Mara kadhaa jogoo yule anayetafutwa anaweza kuhangaisha mtaa mzima, mwisho mnaamua kuwaambia watoto wakamate hata kakuku kadogo ili achinjiwe mgeni, maana muda unapotea. Hivyo, wanaamua kumkamata hata kuku mgonjwa mgonjwa.

Wakati watuhumiwa wakubwa (majogoo) wa ufisadi bado wanaendelea na shughuli zao na wengine kutoweka nchini, wapishi wetu wa serikali ili kujaribu kuonyesha kuwa wanakimbiza kitoweo, wakaamua kukamata vifaranga vya kuku na kwa “mbwembwe” wakatangaza kuwa wamekamata wahusika wa mtandao wa “uchochezi na wa kihalifu”, pale walipowakamata vijana wawili kwa madai ya kuhusika na mtandao wa Jambo Forums.

Kwa kufanya hivyo, kina Jeetu Patel, Vithlani na Gire wameachwa wanadunda mitaani (hata ya Uarabuni) na hata Daudi Ballali (sijui kama mnamkumbuka, aliwahi kuwa Gavana wa Benki Kuu), wote wakiwa wanaendelea na mambo yao. Majogoo yakaachiwa na kuku, tena wa jirani wakakamatwa ilimradi mgeni apewe kitoweo.

Wiki iliyopita, maafisa usalama wa Tanzania wakiongozwa na Mkurugenzi wa Upelelezi, na watu wa Usalama wa Taifa, nusura wamkamate bangusilo (mnyama wa kafara) wa mafisadi. Baada ya kutumia muda mwingi unaolipiwa na fedha za walipa kodi wa Tanzania na vitendea kazi ambavyo vingeweza kutumika kutafuta wezi wa fedha za umma, hasa waliokwapua Benki Kuu, wanausalama wetu wakapoteza muda kujadili kijiwe cha wakesha macho wa Tanzania.

Kwa sababu ambazo Robert Manumba na Rashid Othman wanazijua, Jambo Forums mtandao wa majadiliano huru kuliko mtandao mwingine wowote wa Watanzania kwenye Intaneti, ulikuwa kwenye vinywa vya wanaharakati wengi nchini baada ya vijana wawili wanachama wa mtandao huo kukamatwa na kuhojiwa kwa saa kadhaa kwa madai ya kuhusika na uchochezi na madai mengine ambayo hata kuyaandika yanafanya vidole vigome!

Ninatamani kuandika mengi, lakini najizuia ili niweze kuandika jambo moja tu ambalo Watanzania lazima tuwe macho. Utawala wa mabavu huanza kwa kutishia, kuogofyesha, na hatimaye kuzima sauti za ukosoaji na zipingazo.

Mhanga wa kwanza wa utawala unaoongozwa na mtu mwenye sifa na maarufu, na ambaye ana mvuto mkubwa, ushawishi na ambaye anaamini anaweza kuamuru mbingu zifunguke na ardhi ipasuke, mara zote huwa ni vyombo huru vya habari.

Sitaki kuamini hata kidogo kuwa Tanzania yetu inaweza kuelekea huko. Sitaki kuamini kabisa kuwa kuna watu katika serikali yetu ambao wanaweza kukaa mahali na kupanga kilichopangwa na kujaribiwa kutekelezwa juu ya Jambo Forums.

Kitendo cha maofisa wa usalama kwenda kwenye ofisi ya mtu na kumchukua kwenda naye polisi kufanya naye mahojiano kana kwamba tunaishi katika nchi ya mapolisi ni kitendo cha hatari, na ambacho kama kinaruhusiwa na sheria basi tuna matatizo makubwa.

Haiwezekani polisi amchukue mtu kwenda naye kituoni kwa mahojiano bila amri ya mahakama (warrant) au kuchukua vitu vyake bila amri ya mahakama.

Lakini kuna kitu ambacho ni zaidi ya kukiukwa taratibu. Kwa watu wengi, Jambo Forums walikuwa hawaijui na kwa hakika ni wachache wanaoweza kusema ni wanachama wa forum hiyo.

Tangu kurudi kwa mtandao huo wa http://www.jamboforums.com, zaidi ya wanachama wapya 100 wamejiunga. Bila ya shaka watu wengi waliposikia juu ya Jambo Forums walijiuliza mtandao huo ni nini na kwanini wana usalama waliamua kuuchangamkia ili kuunyamazisha siku chache zilizopita na baadaye kugeuka na kukunja kucha zao?

Yanaweza kutolewa majibu mengi, lakini la kwanza na ambalo nililisema kwenye mahojiano yangu na BBC ni jaribio la kujaribu kuzima maoni yasiyopendeza na yenye kuudhi au kuwakera watawala.

Kuna mawazo ndani ya watawala wetu kuwa, wao ndio viranja wa maoni “sahihi” na yenye kupendeza. Kwa namna fulani wanaamini kuwa wana uwezo wa kuamua ni maoni gani yatolewe na Watanzania.

Aprili mwaka jana, mgongano kama huu ulitokea na ninakumbuka nilichoandika wakati ule kwenye tovuti ya Habari Tanzania kuhusu kauli ya vitisho iliyotolewa na serikali kuhusu baadhi ya vyombo vya habari kufuatia madai ya kutumia lugha isiyofaa.

Nilichoandika wakati ule kwenye gazeti hili hili, naomba nikirudie hapa: “Watanzania tusitetemeshwe wala kutishwa kwa vile watawala wanafikiri wameumbwa kututawala milele na wanaweza kutuchagulia maneno ya kusema.

“Tunakataa hilo, tutaendelea kulikataa na hatuna hofu na vitisho vyao kwa vile wamejitungia sheria ambayo ni wao wanaweza kuitumia dhidi yetu. Hata hivyo, sheria kuu ya nchi yetu ni katiba, na kwa hiyo tunakimbilia ulinzi wake!

“Ni katiba hiyo inayotuhakikishia haki yetu ya kupata na kutoa maoni, si kama hisani ya serikali, bali kama haki ya raia wa Tanzania. Haki ya kutoa maoni si “zawadi” ya Waziri wa Habari, na si “hisani” ya Chama Cha Mapinduzi!”

Hili ni lazima tulirudie tena tunavyoanza mwaka huu, kwani kwa namna fulani kitendo cha kujaribu kuzima forum ya Jambo lilikuwa ni jaribio jepesi la kujaribu kuzima maoni. Lakini pia ninaona kuna sababu nyingine ambayo haihusiani na maoni kwani ni huru, huwa hayafungwi pingu.

Jambo Forums imekuwa chombo ambacho kimeleta vile vilivyofanywa sirini hadharani. Mkataba wa Buzwagi ambao wabunge walinyimwa, ulipatikana kwanza Jambo Forums na hata mkataba wa Richmond ambao matokeo yake ni kutetemesha serikali yetu nao unapatikana hapo.

Ipo mikataba mingine ambayo iko mbioni kuwekwa hata wiki hii na mingine inakera zaidi, na uwezekano wa wananchi wa kawaida hatimaye kuwa na uwezo wa kuona vilivyofanywa sirini unawatisha watawala wetu.

Sasa hivi wanajua wazi kabisa kuwa hakuna jambo lolote ambalo watalifanya sirini ambalo Watanzania hawatajua na hasa kama Jambo Forums itaendelea kuwa hewani. Ninaamini pia walishangazwa sana na habari za kukamatwa vijana wale zilipatikana dakika chache kabla hata hawajafikishwa kituoni na Jambo Forums ikaziweka hewani.

Nina uhakika kuwa kama habari hizo zisingepatikana mapema hivyo, tungekuwa na habari nyingine kabisa ya kuzungumza, kwani sijui kama wangeamua kujitolea habari hizo za kukamatwa vijana hao.

Kwa vile sitaki kusema mengi, na mengi yameshasemwa, naomba kurudia jambo moja muhimu ambalo watawala wetu lazima si tu wakubali, lakini wakubali kuishi nalo. Tanzania imebadilika na Watanzania nao wanabadilika sana. Hawana uwezo tena wa kuzima au kuzuia watu kupata habari na yale mambo ya usiri ya enzi za “ujamaa” hayapo tena.

Wakubali kuishi na teknolojia mpya ya mtandao na wajue kabisa kuwa mtandao unakuja na baraka na laana. Baraka kubwa ni uwezo wa habari kusafiri haraka zaidi kutoka mahali pamoja kwenda pengine, laana kubwa zaidi ya mtandao ni kuwa hakuna siri tena.

Si tu hakuna siri, bali pia hata vinavyodhaniwa kuwa ni siri, si siri tena. Ni jukumu la vyombo vyetu na watunga sheria wetu kufikiri ni jinsi gani wanaweza kuratibu na kusimamia mabadiliko haya.

Hakuna ulazima wa serikali kushinda na raia wake katika mambo ambayo si ya kipaumbele. Wakati waliofuja fedha za BoT bado wanachukuliwa kwa heshima na taadhima, vyombo vyetu vinahangaika na mambo ya Jambo Forums. Binafsi si tu nimeshtushwa, lakini pia nimesikitishwa sana na jambo hili zima.

Ninafahamu kuwa watawala wetu hawajakubali kushindwa na wanapanga mkakati mwingine wa kuishughulikia Jambo Forums au baadhi ya wanachama wake. Wanaweza kuwatumia mawakala au watu wao kujaribu kwa namna moja au nyingine kusambaratisha mtandao huu, ombi langu kwa watawala ni kuwa, kubalini kushindwa ili mtunze heshima zenu.

Wasipofanya madudu kwenye ofisi zao, madudu hayataandikwa kwenye Jambo Forums au forum nyingine, lakini wakiendelea kufanya madudu, wajue wataumbuliwa watake wasitake.

Ni kwa sababu hiyo basi, mafisadi watakapozidiwa wasitafute bangusilo wao kwa kujaribu kufungia Jambo Forums. Kwani safari hii nusura wamkamate bangusilo huyo, lakini kutokana na ushirikiano wa watu wengi wenye kuheshimu haki za raia, uhuru wa mawazo na maoni, bangusilo huyo aliwaponyoka watawala wetu. Ila kwa vile wao ni CCM, sitashangaa watajaribu tena kupata bangusilo mwingine.