Asili na uhalali wa Siku ya Wajinga Duniani
April 1, 2008
LEO ni Siku ya Wajinga Duiani. Siku hii inaadhimishwa kwa watu kufanya matendo wasiyotarajia, kutokana na habari mbalimbali za kushtukiza, kufurahisha na wakati mwingine kuhuzunisha. Baada ya muda fulani, watu hao hujiona wajinga kwa kukubali kudanganywa na jamaa au wapendwa wao.
Uhalisia wa Siku ya Wajinga Duniani hadi sasa haijafahamika, kwani zipo simulizi za kale zinazotolewa na watu mbalimbali kutoka kwenye mtandao, wanaoelezea wajuavyo kuhusu chanzo cha siku hii. Moja ya simulizi hizo zinaeleza kuwa asili ya siku hii ni kalenda ya mwaka 1564 iliyoonyesha kuwa Aprili mosi ya kila mwaka ni wakati wa kusherehekea mwaka mpya, hivyo watu hupumzika. Kalenda hiyo maarufu ilikuwa ya Papa Gregorian iliyotekelezwa kwa tamaduni za Kirumi na Kihindu. Mapumziko hayo yalihusisha pia sherehe za jua kuvuka mstari wa Ikweta, zilizofanyika Machi 21 ambako Waingereza nao waliamua kuifanya siku hiyo kuwa ya wajinga. Inaelezwa kuwa shangwe za siku hiyo zilianza kuadhimishwa katika karne ya 18. Kwa kawaida siku ambayo asili yake bado ni kitendawili hadi leo, baadhi ya watu huitumia kufanya kumbukumbu za wakati fulani huku wengine wakiamini kuwa imetokana na kalenda mpya kwa kuwa awali iliaminika kwamba inapowadia jamii husherehekea mwaka mpya. Pamoja na hayo, Warumi na Wahindu walisherehekea mwaka mpya kati au Aprili mosi ambayo ni siku ya mlingano, yaani jua huvuka mstari wa Ikweta (Machi 20 au 21) na kufanya usiku na mchana kulingana. Hata hivyo, Machi 25 Waingereza hukumbuka tangazo la kupashwa habari kwa Bikira Maria na Gabriel kwamba atamzaa Yesu Kristo kama mwanzo wa mwaka. Aidha, Mwaka 1582, Papa Gregory wa XIII aliagiza kuwapo kwa kalenda mpya na itakayowekwa badala ya ile ya zamani – kalenda ya Julian. Kalenda hiyo ilianza kusherehekewa Januari mosi. Mwaka huo, Wafaransa waliiga mfumo wa kalenda hiyo mpya na kuuweka kwenye kalenda zao ambako mwaka mpya ulisherehekewa Januari mosi. Hii ni kulingana na ufafanuzi wa watu wengi, ingawa baadhi yao wanaendelea kusherehekea Aprili mosi kama siku ya utani. “Pengine walikataa kuipokea siku mpya au hawakusoma kuhusu hilo na wanaendelea kusherehekea mwaka mpya Aprili mosi…kufanya utani kwa tamaduni hizi kuwatuma watu kwenda safari fupi za kuwasumbua – ‘safari fupi za wajinga’ – au kujaribu kumghilibu mtu ili kumwaminisha kitu cha uongo. Hata hivyo mambo hayo yaliendelea kufanyika huko Ulaya,” ilieleza sehemu ya simulizi ya Profesa Joseph Boskin. Ufafanuzi mwingine wa uhalisi wa Siku ya Wajinga Duniani uliotolewa na Profesa Boskin, mtaalamu wa historia kutoka Chuo Kikuu cha Boston, Marekani. Ilieleza kuwa sherehe za siku hii zilianza kipindi cha utawala wa Constantine, wakati kikundi cha uchekeshaji na wajinga cha mahakama kilipomwambia mtawala wa Roma kwamba ni bora kuikimbia falme hiyo. Constantine alimruhusu mchekeshaji aliyeitwa Kugel kuwa mfalme kwa siku moja. “Kwa njia hiyo,” alifafanua Profesa Boskin kupitia simulizi yake na kuendelea kueleza kuwa “Ilikuwa siku makini kwa wakati huo, wajinga walikuwa werevu na wenye busara. Kulikuwa na sheria kwa wachekeshaji kuweka vitu kwa utaratibu wao.” Ufafanuzi huu ulipelekwa kwa jamii na kuvuta hisia kwenye vyombo vya habari kwa kuchapishwa kwenye magazeti mengi mwaka 1983. Magazeti yaliishikilia siku hiyo na kuifanya ijulikane, Profesa Boskin ni miongoni mwa walioifanya siku hii kuwa juu. Lakini ilichukua wiki kadhaa kwa vyombo vya habari kubaini kuwa vilitumika na kuwa waathirika wa siku ya wajinga kwa kujitania wenyewe. Hapa nchini Siku ya Wajinga Duniani huadhimishwa kwa vyombo vya habari hususan redio ambazo wengi husikiliza wakati wa asubuhi kutaka kupata habari mbalimbali. Hutumia muda wa asubuhi kuwaeleza watu wafanye jambo fulani kabla ya saa sita mchana, muda ambao huaminika kwamba unatosha kumsumbua mtu. Siku hii huweza kusababisha foleni kwenye baadhi ya ofisi pale watu wanapokwenda kufuata jambo fulani au kuahidiwa kazi kupitia redio. Lakini wakati mwingine usipokuwa makini hasa kwa wakazi wa mjini, hulazimika kusafiri kutokana na taarifa za ghafla zenye kushtua unazozipokea kutoka kwa ndugu, rafiki ama jamaa yako wa karibu.
Makala hii imeandaliwa na Irene Mark kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari. Wasiliana naye kwa: imarkmeero@yahoo.com.
Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post | TrackBack URI for this post
Comments
Got something to say?

