Annan aisikitikia Kenya
January 27, 2008
KATIBU Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa (UN) ambaye sasa anasuluhisha mgogoro wa kisiasa nchini Kenya, Kofi Annan, jana alitembelea sehemu mbalimbali zilizoathiriwa na machafuko yaliyosababishwa na ghasia za uchaguzi mkuu. Akitumia usafiri wa helkopta kwenda katika maeneo yaliyoathirika na mapigano hayo, alibeba ujumbe wa kulaani ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaoendelea sasa nchini humo.
Katika ziara yake hiyo, alitembelea maeneo ya Eldoret, Rift Valley pamoja na msitu uliochomwa moto wa Molo ambako watu wengi waliuawa.
Katika ujumbe wake huo, Annan alisema mapigano hayo yanaweza kuwa yalisababishwa na uchaguzi, lakini pia yanahusisha vitu vingine.
Alisema ni lazima ukweli utafutwe na wote watakaopatikana na hatia wawajibike.
Wakati Annan akitembelea maeneo hayo, polisi waliokota miili ya watu 16 ikiwa imeungua vibaya huko Nakuru katika Jimbo la Rift Valley.
Mfanyakazi mmoja wa Hospitali ya Nakuru alisema walipokea miili ya watu tisa wanaoaminika kuuawa kwa mapanga, mishale na nondo.
Kundi la vijana wakiwa na mapanga, nondo, mikuki na mishale walionekana wakitoka katika sehemu iliyokuwa ikifuka moshi mzito baada ya kuchoma majengo mengi.
Mauaji hayo yametokea wakati msuluhishi huyo akijaribu kuwapatanisha Rais Mwai Kibaki na hasimu wake mkuu na kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga.
Huku kukiwa na matumaini ya kuendelea vizuri kwa mazungumzo hayo baada ya Rais Kibaki kukutana na Odinga kwa mara ya kwanza Alhamisi wiki hii, kumeibuka shaka ya kukwama kwa mazungumzo hayo baada ya Odinga kutoafikiana na Kibaki kuhusu uundwaji wa serikali ya pamoja kuelekea uchaguzi mkuu mwingine.
Annan pia alipata wasaa wa kukutana na viongozi wa madhehebu ya dini jijini Nairobi na kuzungumzia umuhimu wa maridhiano kwa taifa lao.
“Viongozi hawawezi kufanya hivyo peke yao, kila mmoja anahitaji kushiriki,” alisema Annan.
Kufuatia vurugu hizo, nyumba nyingi zimechomwa moto na mamia ya watu wamekuwa wakimbizi katika makanisa, misikiti na nyumba za marafiki zao.
Taarifa zinaeleza kuwa vijana wengi wa kiume wamekuwa wakiondoka usiku kuzihama sehemu wanazoishi.
Tangu kuanza kwa vurugu hizo zilizosababishwa na uchaguzi mkuu wa Desemba 27, ambako Odinga ametangaza kutoutambua ushindi wa Kibaki, zaidi ya watu 700 wameuawa huku 250,000 wameikimbia nchi.
Blogsphere: TechnoratiFeedsterBloglines
Bookmark: Del.icio.usSpurlFurlSimpyBlinkDigg
RSS feed for comments on this post | TrackBack URI for this post
Comments
Got something to say?

