Aahidi kusikiliza maoni ya watu wote.

December 21, 2007

RAIS Jakaya Kikwete amesema kwamba katika kipindi cha utawala wake atasikiliza maoni na mawazo ya kila mtu, bila kujali itikadi ya chama chake kwa kuwa ni wajibu wake kufanya hivyo ili kujenga demokrasia.

Akizungumza na vyombo vya habari Ikulu, jijini Dar es Salaam wakati wa kuadhimisha miaka miwili tangu aingie madarakani, Rais Kikwete alisema kwamba ni wajibu wa serikali yake kusikiliza kila mtu ili kujenga nchi yenye demokrasia.

“Ni wajibu wetu kusikiliza kila mtu, hata wapinzani wakisema kitu lazima tuwasikilieze. Mimi napokea simu nyingi sana, na nikiona kuna jambo ambalo linahitaji kufanyiwa kazi nalifanya,” alisema Kikwete

Rais Kikwete alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa na mmoja wa waandishi kwamba katika siku za hivi karibuni amekuwa akisikiliza sana wapinzani hususani suala la kuunda kamati ya kuangalia upya mikataba ya madini kwa lengo la kuondoa dosari zilizopo.

Kikwete alisema kwamba wakati wa hotuba yake ya kulizindua Bunge Desemba 30, 2005 mjini Dodoma, aliahidi kuangalia upya mikataba ya madini ili iweze kunufaisha Watanzania, kwani kwa jinsi ilivyo sasa, inawanufaisha zaidi wawekezaji.

Alisema baada ya kuhutubia Bunge, aliunda Kamati ya Masha (Lawrence) ambalo ilijumuisha watendaji wa serikali, lakini baada ya kuona wapinzani wanazungumzia sana suala hilo, akaamua kuunda kamati ambayo itawajumuisha na wengine kutoka katika sekta binafsi ili waweze kutoa mapendekezo yao.

“Tuliona tuondoe hizi kelele za wapinzani, maana wananchi walikuwa wameshaanza kuhisi kwamba serikali haina uchungu na rasilimali za nchi na kwamba tunaziacha zitafunwe tu, takaamua kuwaweka ili nao watoe mapendekezo yao, wapo watu wa serikali katika kamati, lakini wao ni wataalam tu,” alisema Rais Kikwete.

Rais Kikwete alisema kwamba lengo la kamati ni kuangalia ni jinsi gani Watanzania watanufaika na rasilimali za nchi na kuondoa kasoro za awali. “Tanzania Mungu ametupa rasilimali, lakini ametunyima fedha kwa ajili ya kununua teknolojia,” alisema.

Kikwete alisema kuwa alipotamka kule Afrika Kusini kwamba Tanzania ina mpango wa kupitia upya sheria ya madini, alipata simu nyingi sana wakiuliza kwamba nchi inarudi katika kutaifisha mali.

Hivi karibuni, Rais Kikwete aliunda Kamati ya kupitia upya mikataba ya madini, ambayo ilijumuisha wapinzani, maofisa wa serikali na watu kutoka katika sekta binafsi.

Akizungumzia kuhusiana na mipango ya serikali kukamata wahusika wanaojihusisha na rushwa kubwa, Rais Kikwete alisema kwamba mipango imekuwa haina kasi sana kutokana na mazingira magumu ya kupata ushahidi.

Alisema rushwa kubwa inahitaji uchunguzi mpana, unaovuka mipaka ya nchi. “Rushwa kubwa, uchunguzi wake unachukua muda mrefu hadi upate ushahidi wa kupeleka mahakami, ukisikia kwamba mtu fulani kaweka fedha nje, basi lazima upate ushirikiano wa nje kama ilivyokuwa suala la rada, ambalo litafikishwa mahakamani hivi karibuni,” alisema.

Rais Kikwete alisema kwa sasa kuna uchunguzi mbalimbali wa rushwa kubwa unaendelea na utakapomalizika, hatua za kisheria zitafuata.

“Kuna uchunguzi unaendelea, hata suala la rada likifika kortini mtaridhika kwamba kuna kazi imefanyika,” alisema Kikwete.

KUTOKA: MWANANCHI